Marekani-Mexico: Majadiliano ya kirafiki nyakati ngumu
24 Februari 2017Kila kitu kiliashiria urafiki, wakati maafisa wawili wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani walipoizuru Mexico siku za Jumatano na Alhamisi, kiasi kwamba mtu angedhani mataifa hayo mawili yamerejea katika uhusiano wa kawaida. Na wakati wote mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson na wa usalama wa ndani John Kelly walipokuwa Mexico, hakuna alietaja neno "ukuta" hadharani, na hakuna aliesema chochote kuhusu Mexico kupeleka watu waovu tu nchini Marekani.
Lakini pia ziara hiyo haikulenga kuboresha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili ulioharibika tangu Donald Trump alipoingia madarakani mwezi Januari. Tillerson na Kelly walikuwa na malengo ya wastani zaidi, yakiwemo kuzungumza na maafisa wa Mexico na kujaribu kutuliza baadhi ya hofu. Kufikia siku ya Alhamisi, pande zote mbili zilikubaliana kutokubaliana na kuendeleza majadiliano, katika juhudi za kutafuta njia bora za kuendelea kushirikiana katika zama za Donald Trump.
Waziri wa mambo ya nje wa Mexico Luis Videgaray alisema ili kuondoa matusi na hisia hasi vilivyopo sasa, jambo muhimu litakuwa vitendo kuliko maneno. Wakati Kelly na Tillerson walifanya mikutano ya uchangamfu na Videgaray pamoja na mawaziri wa mambo ya ndani na fedha wa Mexico mjini Mexico City, Trump tena alizungumza juu ya jirani huyo wa kusini wa Marekani mjini Washington.
'Masaibu yote ya Marekani ni Mexico'
" Tutakuwa na uhusiano mzuri na Mexico, natumai. Na tusipokuwa nao, hatutokuwa nao," alisema siku ya Alhamisi. Kwa Trump mambo ni rahisi namna hiyo. Kiongozi huyo wa Marekani ameahidi kuurekebisha mkataba wa biashara huru wa mataifa ya Amerika Kaskazini, unaozishirikisha Marekani, Canada na Mexico. Trump ameulaumu mkataba huo kwa kutoweka kwa theluthi mbili ya ajira za viwandani nchini Marekani.
Mjini Mexico City hata hivyo, diplomasia ilifanya kazi. Waziri wa uchumi wa Mexico Ildefonso Guajardo, ambaye hakushiriki katika mazungumzo, alikuwa amesema mkutano na Rais Enrique Pena Nieto utategemea iwapo makubaliano yoyote ya msingi yatafikiwa.
Mwishowe Tillerson na Kelly walikutana na Pena Nieto. Baadhi ya wanasiasa wa Mexico na wafanyabiashara walikuwa na mtazamano kwamba mkutano kati ya rais na mawaziri hao wawili wa Marekani haufai, lakini Mexico inatumai majadiliano yanaweza kutawala. Mwezi Januari Pena Nieto alifuta mkutano na Trump uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 31 mwezi huo kutokana na mipango ya Trump kujenga ukuta kwenye mpaka wa pamoja na kuifanya Mexico ilipie ujenzi huo. Mkutano huo haujapangiwa tarehe mpya.
Mexico imekuwa shabaha ya mabadiliko ya kisera ya Trump kuhusu biashara, uhamiaji na mpaka, na nchi hiyo iliwapokea Tillerson na Kelly kwa mchanganyiko wa hisia za hasira na nia njema. Kama Videgaray mwenyewe alivyotarajia kabla ya ziara hiyo ya ngazi ya juu, lengo lilikuwa kusafisha njia ya kurejesha maelewano ya pamoja.
Kila aliepitia Mexico kurejeshwa Mexico
Karibu kila wiki, jambo jipya la mashaka linaongezwa kwenye orodha ya Mexico. Siku ya Jumanne, wizara ya usalama wa ndani inayoongozwa na Kelly ilichapisha memo mbili mpya zilizozusha wasiwasi kusini mwa Marekani. Marekani ilitangaza mipango ya kuwapeleka nchini Mexico wahamiaji haramu bila kujali utaifa wao, ambao waliingia nchini humo kutokea Mexico.
Hakuna mabadiliko yaliotangazwa kuhusu mipango hiyo. Hata hivyo Videgaray alisema Mexico iliiomba Marekani kutochukuwa hatua za upande mmoja, na Marekani iliahidi kuchukuwa hatua kwa kuzingatia mipaka ya kisheria na kuheshimu haki za binaadamu. "Kila kitu tunachokifanya katika DHS (Wizara ya usalama wa ndani) kitafanyika kisheria na kwa mujibu wa haki za binaadamu katika mfumo wa sheria za Marekani," alisema Kelly.
"Yote haya yatafanyika, kama ilivyo siku zote, kwa ushirkiano wa karibu na serikali ya Mexico," alisisitiza waziri Kelly.
Mamia kwa maelfu ya wahamiaji, wengi wao kutoka mataifa ya Amerika ya Kati, huingia Marekani kinyume cha sheria kutokea Mexico kila mwaka. Mapema wiki hii, katikati mwa awamu mbaya zaidi ya uhusiano wa Mexico na Marekani katika kipindi cha miongo kadhaa, msemaji wa Trump Sean Spicer aliuelezea uhusiano kati ya majirani hao wawili kuwa wa "ajabu" na "imara".
Waziri wa uchumi Guarjado alitumia mzaha kujibu matamshi hayo siku ya Alhamisi, akibainisha kuwa yalikuwa "ukweli mbadala." Hata hivyo milango ya majadiliano kati ya mataifa hayo mawili inaendelea kuwa wazi, na kutakuwepo na mikutano zaidi. "Huu utakuwa mchakato mrefu, na hautakuwa rahisi. Lakini jambo muhimu ni kuchukuwa hatua kuelekea njia sahihi," alisema Videgaray.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae
Mhariri: Saumu Yusuf