Marekani kutoa msaada zaidi wa dola milioni 424 kwa Sudan
25 Septemba 2024Marekani itatoa dola milioni 424 zaidi za msaada wa kibinadamu kuwasaidia watu wa Sudan. Haya yametangazwa leo na balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Thomas-Greenfield.
Greenfield amesema zaidi ya Wasudan milioni 25 wanakabiliwa na njaa kali na takriban milioni 11 wamekimbia makazi yao katika kile ambacho kimekuwa mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.
Balozi huyo pia amesema lazima wazishinikize pande zinazozozana kukubali kusitisha mapigano ili kuruhusu kutolewa kwa msaada wa kibinadamu huko al-Fashir, Khartoum, na maeneo mengine tete, kuondoa vizuizi vya kupelekwa kwa msaada wa kibinadamu katika njia zote na kufanya mazungumzo ya kutafuta amani.
Tangazo hilo linafanya ufadhili jumla wa Marekani tangu kuzuka kwa vita nchini humo kufikia dola bilioni 2.