Marekani kuanza kutoa chanjo ya COVID-19 Jumatatu
13 Desemba 2020Jenerali wa Jeshi la Marekani anayesimamia usambazaji wa chanjo hiyo, Gus Perna, amesema dozi za kwanza zitasafirishwa leo Jumapili na hapo kesho zoezi ya utoaji chanjo litaanza kwa asilimia 100.
Perna amearifu kuwa ifikapo kesho vituo vya kutolea chanjo 145 vitakuwa vimepokea shehena ya kwanza, huku vituo 425 vitapelekewa chanjo siku ya Jumanne na chanjo hiyo itapokelewa pia kwenye vituo vingine 66 siku ya Jumatano.
Kampuni inayotengeneza chanjo hiyo imesema inafanya kazi na washirika wengine kuanza kusafirisha chanjo kwa kutumia magari ya mizigo kutoka kwenye maghala yake yaliyoko kwenye majimbo Michigan na Wisconsin kwenda majimbo yote 50 ya Marekani.
Chanjo hiyo ni lazima ihafidhiwe kwenye baridi ya nyuzi -70 C, hali inayoleta changamoto itakayotatuliwa kwa kutumia barafu na kontena maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi shehena yake.
Watu milioni 3 kupewa chanjo kwenye awamu ya kwanza
Katika awamu hiyo ya kwanza watu milioni 3 watapatiwa chanjo huku watumishi wa afya na wahudumu walio mstari wa mbele watapewa kipaumbele katika utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya corona.
Kampuni ya Pfizer imesema kiasi dozi milioni 25 zinaweza kuwa tayari kwa ajili ya kutimika nchini Marekani ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba. Hivi sasa nchi hiyo imeagiza dozi milioni 100.
Pindi shehena za chanjo zitawasili kwenye vituo vya afya, mamlaka za afya kwenye majimbo na vitongoji vyake ziwachanja watu chini ya muongozo uliyotayarishwa na vituo vya udhibiti magonjwa pamoja na mamlaka ya chakula na dawa.
Utoaji wa chanjo unakuja wakati Marekani imeendelea kuweka rikodi ya juu ya maambukizi na vifo vinavyotokana na virusi vya corona.
Siku ya Ijumaa nchi hiyo ilirikodi vifo vya watu 3,309, na kuvuka idadi ya vifo vya watu 3,124 siku ya Jumatano.
Hicho ni kiwango cha juu kabisa cha vifo kuwahi kushuhudiwa duniani ndani ya siku moja tangu kuzuka kwa janga la Covid-19 mwishoni mwa mwaka uliopita.
Marekani pia ilitangaza maambukizi mapya 231,000 siku ya Ijumaa ambayo ni idadi kuwa kwa siku moja.
Ujerumani kuamua hatua ziada kupambana na COVID-19
Kwengineko kansela Angela Merkel wa Ujerumani anatarajiwa leo kukutana na viongozi wakuu wa majimbo 16 kujadili hatua ziada za kukabiliana na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya corona.
Majadiliano ya leo yatafanyika wakati maafisa wa ngazi ya juu nchini Ujerumani wanatoa wito wa kutangazwa marufuku kali zaidi kudhibiti kuenea virusi vya corona pamoja na rikodi ya juu ya maambukizi inayotia wasiwasi.
Taasisi ya kudhibiti magonjwa nchini Ujerumani ya Robert Koch ilirekodi visa vipya 28,438 katika muda saa 24 zilizopita pamoja na vifo 496 kutokana na COVID-19 idadi ambayo ni kubwa kuwahi kushudiwa nchini humu.
Ujerumani ambayo wakati wa msimu wa machipuko ilikuwa na kiwango kidogo cha vifo ikilinganishwa na mataifa mengine jirani hivi sasa imefikisha idadi ya vifo 21,466 pamoja na maambukizi milioni 1.3 ya virusi vya corona.