Marekani, Korea Kusini zafanya luteka za kijeshi tena
3 Februari 2023Kwenye luteka hizo, wametumia baadhi ya ndege zao za kisasa zaidi, licha ya malalamiko ya Korea Kaskazini kwamba luteka hizo zilikuwa zinazidisha mzozo kwenye rasi hiyo.
Mataifa hayo yamefanya mazoezi ya pamoja ya angani juu ya bahari magharibi mwa rasi ya Korea leo, kwa kushirikisha ndege za kivita kama vile F35A za Korea Kusini, na F-22 na F-35B za Marekani, limesema jeshi la Korea Kusini katika taarifa.
Mwaka uliyopita, Korea Kaskazini ilifanya majaribio yaliovunja rekodi ya makombora ya masafa marefu, ambayo yanapigwa marufuku na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Umoja wa Mataifa.
Jana Alhamisi, wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini ilisema luteka za Marekani na washirika wake zimefikia mstari mwekundu, na zinatishia kuigeuza rasi hiyo kuwa ghala kubwa la silaha na ukanda wa kivita.