Marekani: Baraza la seneti lamwondolea mashtaka Donald Trump
14 Februari 2021Maseneta 57 walipiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa zamani na 43 waliyakaa mashtaka dhidi yake.Wajumbe saba wa chama cha Republican waliungana na wajumbe wa chama cha Democratic kumtia hatiani Trump, lakini idadi hiyo haikufikia theluthi mbili iliyohitajika.
Kiongozi wa maseneta wa chama cha Republican Mitch McConell amesema ni wazi kabisa kwamba Donald Trump alihusika na kuchochea mashambulio kwenye bunge. Hata hivyo hakupiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa hapo awali.
McConell ameeleza kuwa kwa mujibu wa katiba hastahiki kushtakiwa kwa sababu sasa hayumo tena madarakani, hata hivyo Mitch McConnell amesema hakuna tashwishi kwamba Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekosea katika majukumu ya kiuadilifu na kimaadili kwa kuchochea vurugu mbaya mwezi uliopita.
Matokeo ya Trump kuondolewa mashtaka kumesababisha migawanyiko ya utata nchini Marekani kuhusiana na siasa za Trump zilizosababisha maasi dhidi ya mmoja ya mihimili mitatu ya demokrasia ya Marekani.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa rais Joe Biden amesema kipindi hiki cha kusikitisha katika historia ya Marekani kinatukumbusha kwamba demokrasia ni jambo nyeti. Biden amesea ingawa Trump hakutiwa hatiani, kiini cha mashtaka hakiwezi kukanushwa.
Chanzo:AP