Marafiki wa Syria wajadili njia mpya za kuusaidia upinzani
15 Mei 2014Marafiki hao wa Syria wamekutana siku chache tu baada ya mpatanishi wa kimataifa wa mgogoro huo Lakhdar Brahimi kujiuzulu nafasi hiyo, baada ya miaka miwili ya juhudi za kukomesha vita zilizoshindwa kufua dafu, na chini ya wiki tatu kabla ya rais Bashar al-Assad kutafuta muhula wa tatu wa miaka saba.
Jamii ya kimataifa iwangusha wapatanishi
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, alisema Brahimi na mtangulizi wake Kofi Anna walishindwa kupata msaada waliouhitaji kutoka kwa jamii ya kimataifa. Mkutano huo wa mawaziri uliyopewa jina "London 11", ambao unamjumuisha pia waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, ulitarajiwa kuhudhuriwa na kiongozi wa muungano wa upinzani wa Syria Ahmad al-Jarba.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jenipher Psaki, alisema kuna mtazamo mpana kwamba wanahitaji kuongeza mara dufu juhudi nchini Syria, iwe katika kutoa msaada zaidi kwa upinzani, kushughulikia mgogoro wa kibinaadamu, au kuongeza mbinyo kwa utawala wa Syria, na kuongeza kuwa mkutano wa huu unatoa fursa ya kujadili mambo hayo.
Kundi la marafiki wa Syria linazijumlisha nchi za Uingereza, Misri, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Jordan, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na Marekani.
Kabla ya kuondoka mjini Washington, Waziri John Kerry alimlaumu rais Bashar Al-Assad, akimtaja kama kiongozi anaengang'ania madarakani na alietayari kuwaangushia watu wake mabomu ya mapipa, kutumia gesi ya sumu dhidi yao na kuwashambulia kwa mazinga na maroketi, kuwatesa kwa njaa majumbani mwao, na baadae kudai kuwa na haki ya kuiendesha nchi hiyo.
Madai ya mashambulizi ya sumu
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron alitoa msimamo kama huo mapema wiki hii, akirejea kwamba Assad hawezi kuwa sehemu ya wakati ujao wa Syria. Mkutano wa London unaelekea kusisitiza msimamo wa kundi la marafiki wa Syria kuukataa uchaguzi unaoandaliwa na serikali Juni 3.
Mawaziri hao pia wanatarajiwa kuuongezea mbinyo utawala wa Syria kuhusiana na silaha zake za kemikali, baada ya kundi la haki za binaadamu kutoa madai mapya kwamba utawla huo ulitumia gesi aina ya Chlorine. Waziri mkuu Cameron alisema hatua zaidi zitachukuliwa iwapo madai hayo yatagunduliwa kuwa na ukweli.
Watu wasiopungua 150,000 wameuawa katika mgogoro wa Syria, ambao ulianza Machi 2011 kwa maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Assad.
Mmwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe
Mhariri: Josephat Charo