Mapinduzi ya umma Arabuni yaleta machungu
27 Machi 2012Kwa kuwa kutokuridhika kiuchumi kulikuwa na nafasi kubwa sana katika kuibua hasira za mageuzi ya Arabuni, ukuwaji wa uchumi umekuwa kiashirio kikubwa cha ama kufanikiwa au kufeli kwa mapinduzi hayo.
"Katika jamii zenye idadi kubwa ya vijana na ambako kuna haja kubwa ya kutengeneza maelfu ya nafasi mpya za ajira kuhimili nguvukazi inayohitimu kila mwaka, jitihada za kuzisarifu upya sera za kiuchumi katika sekta mbalimbali zina umuhimu mkubwa sana." Anasema Profesa Msaidizi wa Masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Paris, Ziad Majid.
Hiyo ndiyo sababu ni lazima pawe na uendelezaji wa ushirikiano wa kiuchumi, kieneo na kimataifa, katika sekta ya umma na binafsi kwa maslahi ya kipindi hiki kifupi tangu kufanyika kwa mapinduzi ya umma ya Arabuni, na kwa maslahi ya muda mrefu ujao, ili kuzuia uwezekano wa hali kama hii kujitokeza tena.
Mapinduzi ya umma yatia hasara Arabuni
Kwa mujibu wa Shirika la Utalii la Arabuni, ATO, maandamano ya umma yalianza mwaka mmoja uliopita na kusababisha kuporomoka kwa tawala za Tunisia, Misri na Libya, yameugharimu ulimwengu wa Kiarabu kiasi ya dola bilioni 96, asimilia 18 ya hasara hiyo ikitokea kwenye sekta ya utalii.
Katika mataifa ya Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, utalii unachukuliwa kama chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni baada ya fedha kwa wafanyakazi walio nje ya nchi zao. Sekta ya utalii pia inatoa nafasi nyingi za ajira na pia kupunguza utegemezi kwa vyanzo vyengine vya uchumi.
Nchini Misri pekee, kwa mfano, utalii unaajiri takribani wafanyakazi milioni mbili, huzalisha asilimia 11 ya pato jumla la nchi hiyo, na chanzo kikuu cha fedha za kigeni, kikitoa kiasi ya asilimia 20 ya fedha hizo.
Huko Tunisia, utalii hutoa ajira kwa kiasi watu laki nne na kuzalisha asilimia nane ya pato jumla la nchi. Bado ndicho chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa nchi hiyo. Mwaka jana, Syria ilipata zaidi ya dola bilioni nane kwa sababu ya ongezeko la asilimia 40 la watalii waliongia nchini humo.
Kwa ujumla, utalii unamaanisha mengi na makubwa katika uchumi wa nchi za Kiarabu za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati. Bahrain imepoteza kiasi ya dola mia nane baada ya mwaka mmoja wa mtikisiko wa kisiasa katika ufalme huo.
Mapato kutoka nje nayo yapungua
Lakini kuporomoka kwa utalii si changamoto pekee inayoukabili ulimwengu wa Kiarabu hivi sasa. Kuna pia kupanda kwa idadi ya wasio na ajira na kupotea kwa mapato yatokanayo na wafanyakazi wanaoishi nje.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, ILO, kiwango cha ukosefu wa ajira katika ulimwengu wa Kiarabu kilikuwa ni asilimia 10.3 kikilinganishwa na asilimia 6.3 kilichopo kilimwengu. Nchini Misri, ambayo inashikilia nafasi ya tatu katika ulimwengu wa Kiarabu kwa kuwa na watu wengi, kila watu watatu wawili ni vijana walio chini ya miaka 30, na asilimia tisiini ya vijana hao hawana ajira.
Mwaka jana, Faharisi ya Jukwaa la Uchumi Duniani ilibainisha kwamba taasisi husika katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini zimeshindwa kuandaa mazingira ya kiuchumi na kijamii yanayoshajiisha ujasiriamali wa vijana.
Kijana mmoja wa Kimisri aliyehitimu masomo ya biashara, Hassan Massri, ameliambia shirika la habari la IPS na hapa namnukuu: "Mageuzi kama ya mishahara mizuri, na mfumo unaofaa wa elimu na afya ndiyo tunayoyahitaji hapa kwa sasa. Na kuwekeza kwa vijana wajasiriamali kunaweza kutoa njia mbadala kwa vijana wanaomaliza masomo ambao wanaingia soko la ajira lisilokuwapo." Mwisho wa kumnukuu.
Kwa miaka 30 iliyopita, fedha zinazotumwa nyumbani na Wamisri wanaofanya kazi nje zilikuwa chanzo kikuu cha uwekezaji kwenye sekta binafsi, lakini sasa wengi wa wafanyakazi hao wamerudi nyumbani, jambo ambalo Shirika la Wahamiaji la Kimataifa, IOM, linasema litaathiri vibaya uchumi wa nchi hiyo.
Mambo yote haya yakitiwa kwenye kapu moja, jawabu ni kwamba mapinduzi kwenye nchi za Kiarabu yanaweza kuwa yametoa jawabu la nguvu za umma, lakini sio hali ya kiuchumi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/IPS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman