1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yarejea upya Aleppo

23 Oktoba 2016

Mapigano yamerudi upya mjini Aleppo masaa machache baada ya kumalizika muda wa usitishaji mapigano uliotangazwa na Urusi, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali.

https://p.dw.com/p/2RZjv
Syrien Aleppo Bergung Verletzte Ruine
Picha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Afisa mmoja wa Shirika la Msalaba Mwekundu alisema hadi sasa hakuna raia aliyeweza kuondolewa ndani ya siku tatu za kusitishwa kwa mapigano, ambako Urusi ilisema kulikusudiwa kuruhusu raia na majeruhi kuondoka kwenye eneo la mashariki mwa mji wa Aleppo, ambalo linashikiliwa na waasi.

"Kuwaondoa watu hakukuwezekana kwa sababu ya hali mbaya ya usalama kwenye mji huo," alisema msemaji wa shirika hilo nchini Syria, Ingy Sedky, akiongeza kuwa timu ya maafisa wa shirika lake walishindwa kuingia eneo la mashariki mwa Aleppo, ambalo limezingirwa na majeshi ya serikali tangu mwezi Julai, kutokana na makombora yanayorushwa na pia kuwapo kwa wadunguaji kwenye majengo. 

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria lilisema kuwa mwisho wa usitishaji huo wa mapigano ulitandwa na mapigano katika maeneo ya Amiriyeh, Salah al-Din na Sheikh Said. 

Kwa mujibu wa shirika hilo, ndege za kivita zilipaa kwenye eneo la kati la Aleppo na kufanya mashambulizi kwenye eneo moja kwenye viunga vya mji huo, ambako hivi karibuni waasi walikuwa wamevizidi nguvu vikosi vya serikali.

Jeshi la Urusi lilikuwa limetangaza usitishaji mapigano wa masaa 11 siku ya Alhamis ili kuwaruhusu raia, waasi na majeruhi kuondoka kwenye eneo hilo, wakiwaahidi usalama wao. Baada ya hapo, iliongeza muda wa usitishaji huo wa mapigano kwa siku mbili zaidi. Hata hivyo, waasi walisema wasingeliondoka kwenye mji huo.

Upinzani nchini Syria ulisema hakukuwa na hakikisho endapo watakaoondolewa wasingelikamatwa na vikosi vya serikali na wala nafasi ya kuwapa misaada ya kibinaadamu wale wanaobakia kwenye eneo hilo lililozingirwa.

Sedky alisema siku ya Ijumaa kwamba wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu walikuwa tayari kuwaondoa watu kutoka eneo hilo, lakini hawakuwa wamepokea hakikisho muhimu la usalama wao.

Kati ya raia 250,000 na 300,000 wanakadiriwa kuwa wamenaswa mashariki mwa Aleppo, wakiwa hawana chakula wala madawa ya kutosha, huku hospitali zinazowatibu majeruhi nazo zikiwa zinashambuliwa kwa mabomu kutokea angani.

Umoja wa Mataifa wasema Syria yatumia silaha za sumu

Syrien Luftangriffe in Maaret al-Numan
Mtoto aliyesambuliwa kwa siasa za sumu kaika mji wa Idlib, Syria.Picha: Getty Images/AFP/M. Al-Bakour

Wakati huo huo, waangalizi wa Umoja wa Mataifa wamehitimisha kwamba utawala wa Syria ulitumia gesi ya klorini kwenye mashambulizi yake ya tatu ya kemikali mwaka jana. 

Ripoti iliyovuja kutoka Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) hapo Jumamosi (22 Oktoba) inasema kuwa helikopta za serikali ya Syria ziliangusha mabomu ya matangi yakiwa na gesi ya klorini kwenye eneo la kaskazini magharibi mwa mji wa Idlib mwezi Machi 2015.

"Tunaulaani vikali utawala wa Bashar al-Assad kwa kuvunja miiko ya kilimwengu katika matumizi ya silaha za kemikali na ukiukaji wa Syria kwa majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Silaha za Kemikali ambao ilisaini mwaka 2013," alisema msemaji wa Ikulu ya Marekani, Ned Price. 

Marekani imezitolea wito Urusi na Iran kuungana na jitihada za kimataifa za kuiwajibisha serikali ya Syria kutokana na matumizi yake ya silaha za kemikali na kuacha mara moja kuusaidia utawala wa Assad. 

"Ripoti hiyo ya OPCW inathibitisha tukio la tatu la matumizi ya klorini yaliyofanywa na utawala na kuweka wazi ushahidi kwamba serikali ya Assad inatumia kemikali za sumu kwa makusudi, ikivunja sheria za kimataifa," alisema Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power.

Hayo yanatokea wakati Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa likiamua kuanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Aleppo, hatua ambayo inazipa shinikizo serikali za Syria na mshirika wake Urusi, ambazo zimekuwa zikilitwanga kwa mabomu eneo linaloshikiliwa na waasi mashariki mwa Aleppo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Caro Robi