1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Syria

Zainab Aziz24 Septemba 2016

Maeneo kadhaa yanayoshikiliwa na waasi katika mji wa Aleppo zimeshambuliwa na majeshi ya serikali huku juhudi za kidiplomasia kunusuru makubaliano ya kusitisha mapigano zikionekana kugonga mwamba.

https://p.dw.com/p/1K7NQ
Mapigano katika mji wa Aleppo
Mapigano katika mji wa AleppoPicha: picture-alliance/AA/Abaca/E. Leys

Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake London, Uingereza, watu saba wameuwawa ikiwa ni pamoja na watoto.

Mwanachama wa kundi moja la uchunguzi wa ushahidi unaohitajika na mahakama, Mohamed Abu Jaafar, alisema mpaka sasa amerikodi vifo vya wanawake watano na watoto wawili kufikia leo alasiri (23 Septemba), huku akielezea kuwa ni vigumu kujua idadi ya majeruhi.

Shirika la Ungalizi wa Haki za Binaadamu limeelezea kuwa mashambulizi hayo ya angani yamehusisha pia mabomu ya mtawanyo, yakiharibu vibaya vituo vya kutoa huduma ya maji safi, huku misaada ya kiutu iliyokuwa inangojewa mno bado haijafika katika eneo hilo la mashariki ya mji wa Aleppo.

Mashambulio makali yanafwatia tamko la kuanzishwa kwa mashambulizi mapya baada ya kushindwa tena kufikiwa makubaliano ya kidiplomasia ya kusitisha mapigano yaliyotulia kwa kipindi cha wiki moja kabla ya vurugu na vita kuanza tena. Wanaharakati na raia wanasema kwamba mashambulio hayo yalianza tangu siku ya Jumatano usiku na mabomu yamekuwa yanapigwa kiholela bila kujali sehemu za makaazi ya watu.

Uharibifu katika mji wa Aleppo kufwatia mapigano.
Uharibifu katika mji wa Aleppo kufwatia mapigano.Picha: picture-alliance//ZUMA Press/J. Muhammad

Mateso ya raia wa Syria yatakwisha lini?

Hali inaripotiwa kuwa mbaya na majeshi ya anga ya serikali yanaendeleza mashambulio hadi katika maeneo mengine ya mji wa Aleppo. Ibrahim Alhaji mwanachama wa kundi la walinda usalama wa kiraia amesema vituo vyao vitatu vimeshambuliwa katika mashambulizi ambayo huzidi wakati wa usiku.

Hata hivyo, hakuna taarifa zinazowahusu walinda usalama wa kujitolea ambao mpaka sasa wamekwama na hawawezi kusonga mbele. Alhaj ameelezea kuwa kundi lake limeshindwa kwa sababu magari yao yanakabiliwa na uhaba wa mafuta na pia mahitaji yanazidi kiwango cha huduma wanazoweza kutoa. Amesema wametumia muda mwingi kujaribu kuwanusuru watu waliofukiwa kwenye vifusi.

Wakati huo huo, vikosi vya serikali ya Syria vimetoa wito kwa raia waondoke kutoka eneo la Mashariki la mji wa Aleppo na kwenda katika eneo la magharibi ya mji huo ambalo limedhibitiwa na serikali na wameahidiwa kuwa hatotiwa mtu kizuizini wala kuulizwa maswali

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry muda mfupi tu alipotoka kwenye mkutano wa kundi la linalo unga mkono amani ya Syria amesema kuwa bado anayo nia ya kutaka usimamishaji wa mapigano, na kuitaka serikali ya Rais Bashar al-Assad na Urusi inayomuunga mkono kufanya hivyo hivyo.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE
Mhariri: Daniel Gakuba