1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanaendelea Aleppo licha ya pendekezo juu ya kuyasimamisha

Abdu Said Mtullya18 Februari 2015

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anaeushughulikia mgogoro wa Syria amesema amepewa uhakika kwamba majeshi ya serikali yatasimamisha mashambulio katika mji wa Aleppo

https://p.dw.com/p/1Edcp
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anaeushughulikia mgogoro wa Syria Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anaeushughulikia mgogoro wa Syria Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/AA

Mjumbe huyo Staffan de Mistura amearifu kwamba mashambulio hayo yatasimamishwa kwa muda wa wiki sita. Lakini habari zinasema mapambano yanaendelea katika mji huo.

Bwana Staffan de Mistura aliitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya juhudi zake za hivi karibuni za kutafuta suluhisho la kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa atarajiwa tena nchini Syria

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa hapo awali aliupendekeza mpango wa kusimamisha mapigano katika mji wa Aleppo ambao ni mkubwa kabisa nchini Syria. Hata hivyo haijulikani ni lini majeshi ya Syria yataanza kuitekeleza hatua hiyo ya kusimamisha mashambulio katika mji wa Aleppo lakini mjumbe wa Umoja wa Mataifa bwana De Mistura anatarajia kurejea tena nchini Syria haraka kwa kadri itakavyowezekana.

Mjumbe huyo amesema uhakika aliopewa na serikali ya Syria ni uamuzi unaoleta matumaini na amesisitiza juu ya kuutaua mogogoro wa nchini Syria kwa njia ya mazungumzo. Hata hivyo taarifa zinasema tokea jana wanajeshi wa serikali wasiopungua 70 na waasi zaidi ya 80 wamekufa kutokana na mapigano.

Ridhaa ya wapinzani yahitajika

Bwana De Mistura sasa anahitaji kupata ridhaa ya upande wa upinzani,itakayokuwa na maana ya kuwataka wapinzani hao nao wasimamishe mashambulio ya roketi. Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa alikataa kusema lolote baada ya kikao cha faragha cha Baraza la Usalama.

Wakati huo huo mjumbe wa Umoja wa Mataifa anaeushughulikia mogoro wa Syria De Mistura aliwaambia waandishi wa habari anatambua kuwa hali ni ngumu nchini Syria na kwamba yeye haoti ndoto. Hii ni mara ya kwanza kwa bwana De Mistura kutoa taarifa kwenye Baraza la Usalama tokea alipoupendekeza mpango wake wa juu ya kusimamisha mapigano katika mji wa Aleppo mnamo mwezi wa Oktoba. Umoja wa Mataifa unataka kujua jinsi mpango huo ulivyopokelewa na Rais Bashar al -Assad wakati bwana De Mistura alipokutana na Rais huyo mapema mwezi huu.

Mji wa Aleppo umegawanyika katika sehemu mbili.Moja ni ile ya mashariki inayodhibitiwa na serikali na ile ya magharibi inayodhibitiwa na waasi.

Amani katika mji wa Aleppo inaweza kuleta suluhisho nchini Syria

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa De Mistura anataka liwepo eneo huru katika mji wa Aleppo ili kuwezesha misaada kuwafikia watu, kama hatua ya kwanza ya kuleta suluhisho kubwa zaidi la mgogoro wa Syria. Bwana De Mistura amesema matumaini yake ni kwamba mji wa Aleppo unaweza kuwa ishara ya nia nje ya kuleta hali ya kuaminiana na hivyo kuwezesha kuanzishwa tena kwa mchakato wa kisiasa wenye shabaha ya kuleta suluhisho.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afp, dpa,

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman