Mapigano yamepamba moto Idlib na kuwatimua malaki ya watu
16 Januari 2020Wimbi la hivi karibuni kabisa la matumizi ya nguvu lililofuatia hujuma za angani zilizoangamiza maisha ya watu 18 jumatano, limevunja makubaliano ya kuweka chini silaha yaliyotangazwa na Urusi na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki-makubaliano ambayo kimsingi hayajawahi kutekelezwa."Mapigano yameripuka usiku wa manani kusini mwa mji wa Maaret al-Numan, huku mizinga ikifyetuliwa licha ya makubaliano ya kuweka chini silaha kati ya Urusi na Uturuki" amesema Rami Abdel Rahman, mkuu wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam lenye makao yake nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mapigano yamelenga maeneo ya kusini mwa mji wa Maaret al-Numan- kitovu cha mashambulio ya vikosi ya serikali ya Syria.
Wapiganaji wasiopungua 22 wanaoipinga serikali wameuwawa, wengi wao ni wanachama wa Hayat Tahrir al Sham, kundi linalowajumuisha wapiganaji waliokuwa wakishirikiana zamani na mtandao wa kigaidi wa al Qaida nchini Syria.
Baridi kali inayochanganyika na mvua inatishia maisha pia ya wanaokimbia mapigano
Wanajeshi 17 wa serikali na wanamgambo wanaoshirikiana nao, nao pia wameuwawa katika mapigano hayo-shirikia hilo linalosimamia masuala ya haki za binaadam limesema.
Ram Abdel Rahman ameongeza kusema vikosi vya serikali viko umbali wa kilomita saba tu karibu na mji wa Maaret al-Numan, mji ambao ni mojawapo ya ngome za upinzani dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad.
Katika mji wa idlib, raia 18 wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika hujuma za ndege za kivita za Urusi na Syria. Maripota wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, wameshuhudia hali ya vurugu iliyofuatia hujuma hizo zilizovunja majumba kadhaa .
Mustafa anaemiliki duka katika mtaa huo amefanikiwa kuyanusuru maisha yake kabla hujuma hizo kutokea alipoondoka kwenda kutafuta vipuri mtaa mwengine. Ameliambia shirika la habari la AFP aliporejea duka lake limeteketezwa na watumishi wake wanne wamefunikwa na vifusi. Hajasema kama wamenusurika au la.
Mji wa Idlib unahujumiwa mtindo mmoja tangu wiki kadhaa zilizopita na kusababisha maelfu kuyapa kisogo maskani yao. Shirika la Umoja wa Mataifa linalosiimamia huduma za kiutu OCHA linasema tangu decemba mosi iliyopita watu laki tatu wameyapa kisogo maskani yao, wengi wao kutoka kusini mwa Idlib na kuelekea katika maeneo ya kaskazini. Baridi kali inayofuatiwa na mvua inayatia hatarini pia maisha ya maelfu ya watu.