1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapendekezo ya Iran yajadiliwa Geneva

16 Oktoba 2013

Mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran yanatarajiwa kumalizika hii leo.Iran inasema itaridhia ziara za ghafla za wachunguzi wa kimataifa katika vinu vyake vya kinuklea.

https://p.dw.com/p/1A0d9
Wajumbe katika mazungumzo ya Geneva kuhusu mradi wa kinuklea wa IranPicha: Reuters

Baada ya pendekezo "muhimu" lililotolewa na Iran jana,duru ya mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran inamalizika leo mjini Geneva,duru inayoangaliwa kama "kipimo cha mabadiliko ya msimamo wa uongozi mpya wa Iran.

Ishara ya hali mpya iliyozuka mazungumzoni jana ni ule mkutano wa pande mbili kati ya naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya kisiasa Wendy Sherman na naibu waziri mwenzake wa Iran,Abbas Araghschi,uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa wawakilishi watano wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa na Ujerumani jana usiku mjini Geneva."Mazungumzo yalikuwa ya maana" amesema afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani aliyeongeza mazungumzo hayo yataendelea pia hii leo.

Ni nadra sana kuona mazungumzo kama hayo ya pande mbili kati ya Marekani na iran,pembezoni mwa mkutano wa mataifa matano wanachama wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa na Ujerumani pamoja na Iran.Mara ya mwisho mazungumzo kama hao yalifanyika mwaka 2009.

Wendy Sherman Iran Atomgespräch Nuklearprogramm Genf Schweiz
Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Wendy ShermanPicha: Reuters

Mapendekezo mepya yaekwa siri

Mazungumzo ya jana usiku mjini Geneva yamefanyika kuambatana na mawasiliano ya simu waliyokuwa nayo rais Barack Obama na mwenzake Hassan Ruhani wakati wa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New York.

Mjini Washington,msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Jen Psaki amekataa kusema kuhusu mazungumzo hayo ya Geneva hata hivyo amekiri "kwa mara ya kwanza mazungumzo hayo yalikuwa "ya kina" akikumbusha tunanukuu"hakuna anaetegemea maendeleo makubwa kufumba na kufumbua".Duru mazungumzoni zinasema Iran imetoa mapendekezo ya maana ambayo wajumbe wameahidi kuweka siri ili kurahisisha mazungumzo yaendelee vyema.

Akihojiwa na waandishi habari waliotaka kujua kama mapendekezo yaliyowasilishwa na Iran katika mazungumzo ya jana mjini Geneva yanahusu utekelezaji wa itifaki ziada ya mkataba wa kutosambaza silaha za nuklea pamoja pia na suala la kurutubishwa maadini ya Urani,naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran amejibu akisema mada hizo zitajadiliwa katika duru ya leo ya mazungumzo.

Iran Atomanreicherungsanlage
Picha ya satelite ya mtambo wa kurutubisha maadini ya Urani ya iranPicha: AP

Israel yashuku dhamiri za Iran

Itifaki ziada inawaruhusu wachunguzi wa shirika la kimataifa la nishati ya kinuklea kuingia wakati wowote ule kuchunguza vinu vya kinuklea vya Iran.

Israel inaonyesha imeingiwa na wasi wasi na jinsi mazungumzo yanavyoendelea kati ya jumuia ya kimataifa na Iran.Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alilizusha suala hilo jana alipohutubia bunge la Israel Knesset na kuzungumzia uwezekano wa hujuma za kinga za Israel dhidi ya Iran.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman