1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano na juhudi za kidplomasia Syria

Admin.WagnerD22 Februari 2016

Upinzani wa Syria wakutana Saudi Arabia wakati mapambano yakiendelea huku wapiganaji wa jihadi wakidai kuikata njia muhimu ya kufikisha mahitaji kati ya mji wa Alleppo na majimbo mengine yanayoshikiliwa na serikali.

https://p.dw.com/p/1HzzU
Vifaru vya jeshi la Uturuki katika milima nchini Uturuki mpakani na Syria.
Vifaru vya jeshi la Uturuki katika milima nchini Uturuki mpakani na Syria.Picha: picture-alliance/AA/O. Kizil

Monzer Makhous msemaji wa kamati ya ngazi ya juu ya mazungumzo ya upinzani amesema mkutano wao huo unatazamiwa kuendelea kwa siku mbili hadi tatu kuzungumzia hatua zilizofikiwa tokea kundi hilo lilipoamuwa kuhudhuria mazungumzo ya amani mjini Geneva mwezi uliopita.

Mkuu wa kundi hilo Riad Hijab amesema usitishaji wowote ule wa mapigano lazima ufikiwe kwa kuzingatia usuluhishi wa kimataifa na kuzilazimisha Urusi,Iran na wanamgambo wao wa kimadhehebu pamoja na mamluki kusitisha mashambulizi yao.

Leo hii kundi la Dola la Kiislamu na wapiganaji wengine wa jihadi wameikata barabara muhimu ya kufikisha mahitaji yenye kuunganisha mji wa magharibi wa Syria wa Allepo na maeneo mengine yanayoshikiliwa na serikali.

Barabara hiyo kati ya Allepo na mji wa Khansser kusini mashariki ni njia pekee inayotumiwa na vikosi vya serikali na raia wanaoishi katika vitongoji vinavyodhibitiwa na serikali kusafria kwenda kwenye majimbo ya karibu.Hali hiyo itapelekea hali ya uhaba wa maji na chakula kuzidi kuwa mbaya kwa raia.

Hakuna uwezekano wa kuingilia kieshi Saudi Arabia na Uturuki

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema amefuta uwezekano wa nchi yake na Saudi Arabia kufanya operesheni ya kijeshi ya nchi kavu nchini Syria kwa kusema kwamba hatua yoyote ya kijeshi ya ardhini itabidi ihusishe nchi zote washirika.

Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu.
Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu.Picha: AFP/Getty Images/A. Altan

Cavosoglu amesema "Iwapo kutakuwa na operesheni ya ardhini inapaswa ifanywe kwa pamoja na nchi zote washirika.Ukweli ni kwamba tumeshindwa kupambana na kundi la Dola la Kiislamu. Nchi 65 duniani zimeshindwa kupambana na Daesh kwa sababu hakuna mkakati, hakuna nia."

Akizungumzia makubaliano ya muda yaliofikiwa na Marekani na Urusi kusitisha uhasama nchini Syria waziri huyo amesema mashambulizi ya anga ya Urusi nchini Syria ni kikwazo kikubwa cha kufanikisha usitishaji wa mapigano nchini Syria.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema leo mashambulizi kadhaa ya kujitowa muhanga mwishoni mwa juma yaliouwa zaidi ya watu 140 yanayodaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria yamenuwia kuvuruga machakato wa amani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Yusuf Saumu