1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho ya Vitabu ya Frankfurt yafunguliwa rasmi

Erasto Mbwana18 Oktoba 2005

Maonyesho ya kimataifa ya 57 ya vitabu mjini Frankfurt, Ujerumani yatafunguliwa leo rasmi na Waziri Mkuu wa Korea ya Kusini Lee Hae-Chan na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani anaye ng’atuka Joschka Fischer.

https://p.dw.com/p/CHeZ
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Joschka Fischer
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Joschka Fischer

Maonyesho ya vitabu ya mwaka huu yamevunja rekodi ya Waonyeshaji. Waonyeshaji 7,223 kutoka nchi 101 wataonyesha vitabu vyao vipya vipatavyo 380, 655.

Kauli mbiyu ya mwaka huu ni Korea kwani kwa kawaida kila mwaka Maonyesho haya huteua nchi moja ambayo huwa mgeni wa heshima. Itakumbukwa kuwa Afrika ilikuwa mgeni mahsusi mwaka 1980.

Korea inawakilishwa na Wandishi 62 wa vitabu na hasa kutoka Korea ya Kusini. Wengi wao wameteswa kutokana na juhudi zao za kupigania muungano wa Korea mbili zilizotengana.

Ingawaje Wandishi wengi wa vitabu, vitabu vyao vinavyoonyeshwa kwenye Maonyesho ya Frankfurt wanafahamika sana, lakini kinyume chake, Wandishi wengi kutoka Korea ni wapya katika masoko ya vitabu ya Ulaya.

Mwandishi wa Vitabu ambaye pia ni Mkurugenzi wa ujumbe maalumu, Hwang Chi-Woo amesema, “Korea haijulikani sana barani Ulaya. Utamaduni wa Korea umefunikwa na Japan na China.”

Mkurungenzi wa Maonyesho ya Vitabu, Jürgen Boos, amezungumzia kuhusu nafasi maalumu ya utamaduni wakati wa Maonyesho.

Amesema kuwa ingawaje kipaumbele cha Maonyesho ya Vitabu, ambayo ni makubwa sana ulimwenguni ni maslahi ya kiuchumi na kujipatia faida ili gharama za harakati zake ziweze kurudishwa lakini pia matafrija ya kiutamaduni yanapewa umuhimu mkubwa.

Maonyesho ya Vitabu ya Frankfurt yatafungua milango yake kwa Wafanyabiashara kuanzia kesho Jumatano na Jumamosi na Jumapili watu wa kawaida wataruhusiwa kuyaona.

Kilele cha Maonyesho kitakuwa Jumapili ijayo ambapo Mwandishi mashuhuri wa vitabu wa Kituruki, Orhan Pamuk, atatunukiwa tunzo la Amani la Wachapishaji na Wauzaji wa Vitabu nchini Ujerumani katika Kanisa la Mtakatifu Paulo mjini Frankfurt.

Dibaji ya Tunzo hilo linaloambatana na Euro 15,000 inasema, “Wakfu unatambua umuhimu wa amani, utu na maelewano kati ya watu. Kwa hiyo, anayetunukiwa tunzo hili amefanya makubwa katika fani za uandishi fasihi, sayansi, utamaduni na kuendeleza amani. Tunzo hili hutolewa bila ya kujali taifa la mtu, rangi yake, dini yake au imani yake.”

Mwandishi wa Vitabu Pamuk, anakabiliwa na kifungo nchini Uturuki kwa kuandika kuhusu mauaji ya halaiki ya Waarmenia yaliyofanywa wakati wa utawala wa ufalme wa Ottoman.

Ameikasirisha serikali ya Uturuki wakati alipoliambia gazeti moja la Uswissi, “Waarmenia na Waturuki millioni moja wameuawa katika nchi zao na hakuna hata mtu mmoja anayethubutu kusema hivyo isipokuwa mimi.”

Atafikishwa mahakamani mwezi wa Desemba mwaka huu na kujitetea mashtaka ya kudhalilisha uzalendo wa Kituruki.

Miongoni mwa Wafrika waliowahi kutunukiwa Tunzo hilo la Amani ni hayati Rais Leopold Sédar Sengor wa Senegal mwaka 1968 na Chinua Achebe wa Nigeria mwaka 2002.

Mshindi wa zawadi mpya ya uandishi fasaha wa riwaya kwa lugha ya Kijerumani ya Chama cha Wachapishaji wa Vitabu vya Kijerumani ni Arno Geiger kutoka Austria.

Ametunukiwa tunzo hilo kwa kitabu chake kilichopewa jina la “Es geht uns gut” maana yake ikiwa “Hatuna shida.”

Tunzo hilo linaloandamana na Euro 25,000 litatolewa kila mwaka katika Maonyesho mashuhuri ya Vitabu yanayofanyika mjini Frankfurt.

Lengo lake ni kutangaza ulimwenguni kote vitabu vya lugha ya Kijerumani.