1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Mengi yamefanywa,tija hakuna

14 Mei 2014

Kimantiki,kujiuzulu mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu kwa Syria Lakhdar Brahim ni matokeo ya kushindwa juhudi zake nchini humo

https://p.dw.com/p/1Bzk5
Rainer Solliich wa idhaa ya kiarabu ya DWPicha: DW/P. Henriksen

►Sifa za mwanasiasa zinategemea anachokisema na anachokitenda-zaidi kuliko yote lakini inategemea ufanisi wa juhudi zake. Lakhdar Brahimi,akiwa mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa kwa Syria hakufanikiwa pakubwa,sawa na mtangulizi wake Kofi Annan.Amejaribu kupatanisha,amejaribu kuzileta katika meza ya majadiliano pande zinazohasimiana.Amejaribu kwa kadri ya uwezo wake kuzishinikiza pande zinazohusika. Lakini juhudi zote hizo hazikusaidia kitu

Watu wasiopungua laki moja na 50 elfu wameuwawa,wengine wanaokadiriwa kufikia milioni tisa wameyapa kisogo maskani yao na ufumbuzi wa kisiasa hauna dalili ya kupatikana.Kila siku mabomu yanaripuliwa na watu kuuliwa.Na kuna dalili kubwa zinazoonyesha kwamba serikali pengine imetuimia gesi za sumu dhidi ya raia.

Kwa maneno mengine Lakhdar Brahimi hajafanikiwa lolote nchini Syria -kwa hivyo uamuzi wa kujiuzulu uliokuwa ukisubiriwa tangu zamani-kimantiki ni matokeo ya hali yote hiyo.Kwamba waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wegineo, wanamvulia kofia ,licha ya juhudi zake kushindwa kuleta tija, ni jambo linaloeleweka. Brahimi hakubakisha la kufanya. Na hatimae alikuwa mkweli na kufika hadi ya kuwaomba radhi wananchi wa Syria kwa kushindwa juhudi zake.

Kilio cha wananchi wa Syria ni kutaka vita vikome na sio zaidi

Tangu awali, mwanadiplomasia huyo wa kutoka Algeria alilitaja jukumu alilokuwa ametwikwa kuwa " ni jambo lisilowezekana". Aliyoyasema Brahimi yamejitokeza kuwa kweli na ukweli huu hata atakaechaguliwa badala yake hatokosa kuugundua. Si serikali ya Bashar al Assad wala si sehemu kubwa ya makundi ya upinzani, hakuna anaependelea kwa dhati ufumbuzi wa kisiasa. Assad,licha ya kujikuta kati kati ya vita anajibwaga katika kiini macho cha kidemokrasia kwa kuitisha uchaguzi wa rais katika wakati ambapo vikosi vyake vinavurumisha mabomu mitaani. Upande wa upinzani nao makundi ya itikadi kali ya dini ya kiislam yanayoshirikiana na mtandao wa Al Qaida yanazidi kupata nguvu na kuwatia katika hali ya vitisho na dhiki pia raia.

Hata katika medani ya kimataifa hakuna ishara ya kupatikana ufumbuzi wa haraka.Iran na hasa Urusi wanazidi kumlinda muimla wa Syria na kumuunga mkono kifedha na kijeshi.Mataifa kadhaa ya magharibi na nchi za ghuba zinaunga mkono baadhi ya makundi ya upinzani. Uungaji mkono huo lakini hautoshi kuwapatia ushindi wa kijeshi dhidi ya serikali ya mjini Damascus. Kuingilia kijeshi nchi za magharibi dhidi ya ridhaa ya Moscow ni muhali ukizingatiwa mzozo wa Ukraine. Kwa wananchi wa Syria, ni sawa tu nani atateuliwa kushika nafasi ya Brahimi-hawahitaji mjumbe maalum,wanahitaji jumuia ya kimataifa au dola kuu litakalomaliza vita nchini mwao.

Mwandishi: Rainer Sollich/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef