1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya5 Novemba 2013

Wahariri leo wanatoa maoni juu ya kesi inayomkabili aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi,na pia wanazungumzia juu ya kuchujuka kwa Rais Obama katika nyoyo za watu duniani.

https://p.dw.com/p/1ABhR
Aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi
Aliekuwa Rais wa Misri Mohammed MursiPicha: Reuters

Wahariri pia wanatoa maoni juu ya matata yanayomkabili Mwenyekiti wa timu maarufu ya kandanda duniani FC, Bayern Munic,Uli Hoeneß.

Juu ya kesi ya aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linatilia maanani kwamba mahakimu kwa sasa wameyapunguza makali kwa kuiahirisha kesi ya Mursi hadi mwezi januani mwaka ujao.

Mhariri wa gazeti hilo anasema uamuzi wa kuiahirisha kesi hiyo italeta utulivu nchini Misri na pia katika jumuiya ya kimataifa.Lakini jambo muhimu kwa utawala wa kijeshi nchini Misri kutambua, ni kwamba kesi inayomkabili Mursi ndiyo itakayotumiwa kama kipimo cha dhamira ya utawala huo katika kuleta demokrasia ya dhati.

Rais Obama

Rais Barack Obama amechujuka katika nyoyo za watu duniani. Alivyoanza,sivyo alivyo sasa.Hayo ni maoni ya mhariri wa gazeti la "Bild". Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Obama alijaa katika nyoyo za watu duniani. Aliwakilisha matumaini. Katika dunia iliyojaa udhalimu, vita na mauaji, Obama aliahidi kuleta amani, demokrasia na haki."Alituahidi kuifunga jela ya Guantanamo". Kutokana na ahadi hizo Obama alitunukiwa nishani ya amani ya Nobel. Lakini lahaula,jela ya Guantanamo bado imesimama palepale. Obama amekuwa kiranja wa mauaji .Na inavyoelekea mwili wake hautetemeki anapotoa amri ya kuua.Jee Huo ni mwisho wa mwanasiasa aliekuwa mfano wa kuigwa.?

Mhariri wa gazeti la "Bild" anasema Obama sasa anapaswa kukigeuza kibao.Lazima arejeshe imani ya hapo awali, katika nyoyo za watu.Dunia bado inamhitaji. Ikiwa atashindwa, basi maadui wa amani na demokrasia watalivaa taji la ushindi.

Uli Heoneß na dafina ya michoro ya wasanii

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linatoa maoni juu ya Mwenyekiti wa klabu maarufu ya kandanda duniani, F.C Bayern Munic, Uli Hoeneß .Atafikishwa mahakamani kuyajibu mashtaka ya kukwepa kulipa kodi.

Gazeti hilo linasema ni kweli,haitarajiwi kwamba Uli Hoeneß atakula miaka jela.Lakini itakuwa vigumu hata kwa wapambe wake kumshauri andelee kuwa mwenyekiti wa FC Bayern Munic. Na mhariri wa "General -Anzeiger "anazungumzia juu ya michoro ya wasanii maarufu iliyotekwa na mafashisti wakati ya vita kuu vya pili. Picha hizo ziligunduliwa na maafisa wa idara husika ya serikali katika makaazi machafuchafu katika mji wa Munic mnamo mwaka wa 2010. Katika maoni yake gazeti la General -Anzeiger linauliza kwa nini dafina hiyo haikuchapishwa hadharani tokea wakati huo?

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef