1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatawania muhula mwingine

7 Juni 2016

Wahariri wanatoa maoni juu ya uamuzi wa Rais wa Ujerumani Gauck wa kutowania muhula mwingine.Wahariri pia wanatoa maoni juu ya hatari ya mashambulio ya kigaidi wakati wa michuano ya kandanda mjini Paris

https://p.dw.com/p/1J1p6
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck
Rais wa Ujerumani Joachim GauckPicha: picture-alliance/dpa/H. Schmidt

Juu ya uamuzi wa Joachim Gauck wa kutowania muhula mwingine wa urais, mhariri wa gazeti la "Münchner Merkur" anasema jambo la kulitilia maanani ni changamoto ya kumtafuta mjumbe madhubuti wa kumwakilisha Kansela aliedhoofika.

Mhariri huyo anasema baada ya Joachim Gauck kuondoka atahitajika mjumbe atakaeweza kuvileta pamoja vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU na CSU.

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" pia linasema atakaemfuatia Gauck atapaswa kuwa na uwezo wa kuishikilia nchi pamoja. Lakini mhariri huyo anauliza, jee ni nani anaeweza kujipiga kifua na kujitokeza mbele ili kuikabili changamoto hiyo?

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaamini kwamba Rais Joachim Gauck anayo mengi zaidi ya kusema, kwa sababu muda wake wa kuwemo kitini bado upo. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha juu ya miito ya busara aliyoitoa kusisitiza maadili ya kibinadamu.

Mhariri huyo anasema Gauck alitoa mfano thabiti katika kuhimiza maadili ya uhuru wa mwanadamu, mshikamano na kazi za kujitolea zinazofanywa na raia. Gazeti la "Lausitzer linasema Gauck ametimiza kazi nzuri na atakaemrithi atapaswa kujenga zaidi katika msingi huo.

Mashambulio ya kigaidi

Maafisa wa usalama nchini Ukraine wamemkamata nchini humo, raia mmoja wa Ufaransa anaetuhumiwa kuwa gaidi. Kwa mujibu wa taarifa mtu huyo alikuwa anapanga mfululizo wa mashambulio ya kigaidi wakati wa michuano ya kandanda ya kugombea ubingwa wa Ulaya.

Matayarisho ya ulinzi mkali wakati wa mashindano ya kandanda
Matayarisho ya ulinzi mkali wakati wa mashindano ya kandandaPicha: picture-alliance/dpa/T.Vandermersch

Juu ya mtuhumiwa huyo gazeti la "Neue Osnabrücker " linasema ingawa hayajapatikana maelezo zaidi juu ya silaha alizokutwa nazo mtu huyo, jambo moja ni wazi kabisa, kwamba hatari ya kufanyika mashambulio ya kigaidi barani Ulaya iko kweli. Gazeti hilo linaeleza kwamba pana uhusiano kati ya kukamatwa kwa mtu huyo na tishio dhidi ya mashindano ya kugombea ubingwa wa Ulaya mjini Paris.

Mhariri wa " Neue Osnabrücker " anatahadharisha kuwa mkasa huo unapaswa kuwa onyo kwa idara za usalama barani Ulaya. Kwa muda mrefu hatari kutokea kwenye makundi mengine mbali na "Dola la Kiislamu" imekuwa inapuuzwa na idara za usalama za nchi za Ulaya.

Erdogan aendesha kampeni ya chuki

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linazungumzia juu ya kampeni ya chuki inayoendeshwa na Rais wa Uturuki,Tayyip Erdogan dhidi ya mbunge mmoja wa Ujerumani mwenye nasaba ya kituruki. Erdogan amedai kuwa mbunge huyo amesimama karibu na magaidi.

Yafaa kutilia maanani kwamba Bunge la Ujerumani Alhamisi iliyopita lilipitisha azimio la kuyatambua mauaji ya watu wa Armenia kuwa ya halaiki. Mhariri wa gazeti hilo anasema Erdogan anafikiri kuwa anayo haki ya kuwatawala watu wote wenye nasaba ya kituruki duniani kote.

Mhariri huyo anasema Erdogan anajiona kuwa ni Sultani wa Waturuki wote, pia wale wanaoishi nchini Ujerumani. Na Sultani hataki kupingwa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu