1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mkutano wa kuutatua mgogoro wa Ukraine

Abdu Said Mtullya17 Aprili 2014

Pamoja na masuala mengine wahariri wanauzungumzia mkutano wa mjini Geneva juu ya mgogoro wa nchini Ukraine.Na pia wanauzungumzia umaarufu wa Ujerumani duniani.

https://p.dw.com/p/1Bk2I
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Sergei Lavrov wa Urusi wakutana Geneva
Mawaziri wa mambo yanje wa Marekani John Kerry na wa Urusi Sergei Lavrov wakutana GenevaPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Der neue Tag" linatoa maoni juu ya mkutano unaofanyika mjini Geneva leo ambako wajumbe kutoka Marekani, Urusi,Ukraine na Umoja wa Ulaya watajaribu kuutatua mgogoro wa Ukraine.

Katika maoni yake Mhariri wa gazeti hilo kwanza amemnukuu Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliesema kwamba mkutano huo haupaswi kushindwa.

Hata hivyo Mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anakumbusha juu ya mgogoro wa Syria na msimamo wa Rais Putin.Lakini anaeleza kwamba kwa kutaka kuzirejesha enzi za kisoviet, Putin inajiingiza katika matatizo ya fedha na ya kiuchumi.

Gazeti la"Der Neue Tag" linaeleza kwamba tokea kuanza kwa mgogoro wa Ukraine,akiba ya fedha ya Urusi imepungua hadi kufikia Dola Bilioni 500. Kwa usemi mwingine akiba ya fedha ya Urusi imepungua kwa asilimia 10. Zaidi ya hayo, anasema mhariri wa gazeti hilo, thamani ya sarafu ya Urusi, Ruble,imepungua kwa asilimia 20 mbele ya Euro. Na kwa hivyo hoja hizo zinaweza kuwa muhimu kwenye mkutano wa mjini Geneva.

Majeshi na sihaza zaidi za NATO

Gazeti la " Augsburger Allgemeine" linatoa maoni juu ya uhusiano baina ya mfungamano wa kijeshi wa NATO na Ukraine kwa kusema kuwa ni kweli kwamba Urusi inacheza mchezo fulani nchini Ukraine,kiasi cha kuzipuuza sheria za kimataifa. Lakini kwa sasaUrusi haizihatarishi nchi za Ulaya ya mashariki ambazo ni wanachama wa NATO. Na chembelecho, Ukraine siyo mwanachama wa NATO.Na kwa hivyo uamuzi wa Nato wa kupeleka silaha na majeshi zaidi katika nchi za Ulaya mashariki siyo wa lazima-na kwa kweli hautaleta manufaa.

Ujerumani ni maarufu sana duniani

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la utangazaji la Uingereza BBC, umebainisha kwamba Ujerumani ndiyo nchi inayopendwa zaidi kuliko nyingine yoyote duniani. Lakini, jee inapaswa kuitimiza dhima gani kutokana na umaarufu huo? Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema kwa Ujerumani kuwa nchi inayopendwa kuliko nyingine yoyote duniani, kunaandamana na wajibu. Yeyote anaependwa anapewa imani na wengine. Na yeyote anaependwa, yeye amepevuka katika kuyatekeleza majukumu fulani,kwa nia ya kujenga.

Ujerumani inapaswa kutoa mchango wake katika diplomasia ya dunia,kwa kusuluhisha baina ya pande ambazo bado zinavutana duniani. Umaarufu unaipa Ujerumani majukumu. Haina maana kwamba kila kitu kimeenda sawa.Iko sababu ya kuboresha, lakini hakuna sababu ya kushika tama.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri: Josephat Charo