Maoni: Wajibu wa Ujerumani waendelea
27 Januari 2019Imechukuwa muda mrefu kwa Ujerumani hatimaye kukiri kwamba ni taifa la uhamiaji. Wengi bado wanakataa kutambua kwamba ni uimarishaji wa utamaduni ikiwa watu kutoka duniani kote wanataka kuishi na kufanyakazi nchini Ujerumani. Kwa kuzingatia maendeleo ya muundo wa watu, raia wa taifa hilo lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya hawataweza kuendeleza kiwango chao cha maisha bila ya nguvu kazi na ujuzi wa watu kutoka mataifa mengine.
Dhamira ya wazi
Hii leo, miaka 74 kuelekea siku ambayo kambi ya mateso ya Auschwitz ilikombolewa, ni siku nzuri ya kutafakari juu ya nini inamaanisha kuhamia Ujerumani, kuishi hapa na hata kutamani kupata uraia wa Ujerumani.
Ni siku nzuri kuzingatia kwa nini dhamira ya kuwa nchi ya uhamiaji inajumlisha sheria zilizo wazi zaidi na zisizobadilika. Na kwamba kujielewa kwetu kama Wajerumani hakupaswi kamwe kujadiliwa, mahala ambako hakuwezi kuwa na muafaka.
Ujerumani inabeba jukumu la mauaji ya Wayahudi wasiopungua milioni 6. Inabeba jukumu la vifo na mateso ya mamilioni kadhaa ya watu wengine barani Ulaya na zaidi ya hapo. Ukurasa huu wa historia ya Ujerumani haupaswi kamwe kufikia mwisho, haupaswi kamwe kusahaulika na unapaswa kuendelea kupitia siku za kumbukumbu kama leo.
Lakini katika kutazama nyuma, hatupaswi kujifunga katika ukatili wa wakati uliyopita. Badala yake, tunapaswa kutazama mbele na kuendelea kuuliza nini tunapaswa kufanya sasa, leo, ili kuutendea haki wajibu huu hasa.
Kimsingi ni kwa sababu manusura wa mwisho, lakini pia watendaji wa mwisho wa ukatili huu, wanakufa, ndiyo maana tunapaswa kutafuta njia za kuwafanya vijana wawajibike, kwani wao ndio wapigakura wa baadae, na watoa maamuzi ya kisiasa wa baadae.
Kadiri utawala wa Wanazi unavyofutika na kuzikwa kwenye kaburi la sahau, ndivyo inavyozidi kuwa vigumu kuweka hai umuhimu wake katika wakati wa sasa. Hivyo ndivyo mambo yalivyo.
Kila chama sawa
Hivyo ni muhimu na sawa kutoa taarifa katika shule, kuandaa safari za shuleni kuzuru mojawapo ya kambi za mateso au maangamizi, lakini pia kutembelea viwanja vya vita vya Verdun. Ni muhimu na vizuri kwamba nguvu za kidemokrasia na kisasa zimeungana zaidi ya mipaka ya kivyama ili kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi.
Lakini ni muhimu pia kuweka wazi kwa wale ambao mababu zao hawakuishi hapa wakati wa kipindi hicho cha kiza zaidi katika historia ya Ujerumani, au ni wahamiaji wapya, kwamba kila anaeishi nchini Ujerumani leo anapaswa kuwa tayari kubeba dhamana hii. Haihusiki kwa namna yoyote na hatia ya mtu mmoja, lakini na utambulisho wa kitaifa wa Ujerumani. Ufafanuzi huu pia kumbukumbu za leo ni mahala pake.
Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Oummilkheir Hamidou