1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uislamu wa dhati wa Ulaya hauna mbadala

Sabine Faber13 Januari 2015

Tangu mashambulizi ya Paris, mjadala juu ya kuuhusisha Uislamu na vurugu umepamba moto Ujerumani. Lakini mjadala huu unapuuza maono ya mafanikio ya uraia wa Uislamu katika taifa hili, anasema Loay Mudhoon.

https://p.dw.com/p/1EJHz
Aktionstag der deutschen Muslime 19.9.2014 Muslime gegen Hass
Picha: Getty Images/Sean Gallup

Ni dhahiri kuwa mashambulizi ya mjini Paris yameibua maswali yanayoeleweka: Je, Uislamu katika msingi wake ni dini isiyo ya kiutu na inayounga mkono ukatili? Je, mandishi makuu ya dini hii ya ulimwengu yanahalalisha mbinu ya matumizi ya nguvu iliyopitiliza kama inavyoonekana kwa makundi ya jihadi? Na muhimu zaidi ni je, sera ya ushirikishwaji wa Waislamu nchini Ujerumani imeshindwa?

Kwa hakika maswali hayo ni ya haki. Lakini yanapuuza kiini cha tatizo, ambacho ni suala la utangamano wa Uislamu na mafanikio ya kisasa na jamii huru ya kidemokrasia. Lazima ifahamike kwamba hakuna kitu kama Uislamu usiyobadilika. Hakuna mahala popote duniani ambako Waislamu wote wanakuwa na mtazamo sawa.

Global Media Forum Workshop Terroristen im Netz Loay Mudhoon
Mwandishi wa DW Loay Mudhoon.Picha: DW

Katika taifa lolote la Kiislamu, kuna Uislamu tofauti unaofuatwa na kutekelezwa. Kwa mfano, kuna tofauti kubwa kati ya Uislamu nchini Saudi Arabia na ule unaotambuliwa na serikali ya Washia waliowengi nchini Iran. Na katika mataifa ya Kiislamu yaliyofanikiwa kiuchumi kama vile Uturuki na Malaysia, kumejengwa aina ya Uislamu wa wastani wa kihafidhina.

Ukweli huu kuhusu Uislamu unabainisha wazi kuwa ni Waislamu wenyewe wanaoamua juu ya kile wanachokitafsiri kuwa ni Uislamu kulingana na wapi na vipi wanaishi. Uislamu wa madhehebu ya Sunni unaofuatwa na walio wengi zaidi, hauna uongozi wa juu na hauna uamuzi wa mwisho kama alivyo papa katika kanisa kotoliki. Na hili linatuongoza kwenye swali muhimu la msingi, ambalo tunapaswa kujiuliza kufuatia mashambulizi ya Paris: Ni Uislamu gani hasa tunapaswa kuwa nao barani Ulaya?

Mafanikio ya sera ya kuutangamanisha Uislamu na utamaduni wa Ujerumani

Kutokana na mjadala uliojaa jazba na mabishano, tuko katika hatari ya kupoteza dira ya mafanikio muhimu ya miaka ya karibuni. Kwa sababu kupitia kuingizwa kwenye katiba, Mkutano mkuu wa Waislamu wa Ujerumani DIK mwaka 2005, na kuanzisha mchakato wa kutangamanisha Uislamu na sheria yetu ya msingi, kumekuwa na mabadiliko makubwa sana katika uelewa wa serikali ya Ujerumani kuhusu Uislamu.

Licha ya mivutano na malumbano ya hapa na pale, mchakato huu wa mjadala wa wazi baina ya serikali na raia wake Waislamu, umesaidia kubadili sura ya Uislamu nchini. Hata kama makundi yanayotafuta umaarufu yanautusi Uislamu mara kwa mara na kuutumia kujenga hofu miongoni mwa raia, mafanikio ya sera ya ushirikishwaji hayawezi kukanushwa.

Na hivi sasa tumeshapiga hatua muhimu mbele,kuanzisha masomo ya dini ya Kiislamu katika shule za serikali majimboni. Uanzishwaji wa fani ya theolojia ya Uislamu katika vyuo vikuu vya ndani ni jambo la matumaini na litakuwa nyenzo muhimu ya kujenga Uislamu unaowiana na misingi ya demokrasia ya Ulaya nchini Ujerumani na katika mataifa mengine ya Ulaya.

Kwa sababu Uislamu mara zote umekuwa ukijiambatanisha na wakati wake, na theolojia ya uislam ni matokeo ya nguvu ya kisiasa, serikali na jamii hazina budi kuhakikisha kuwa mchakato wa kujenga Uislamu unaowiana na utamaduni wa Ulaya unaharakishwa. Kwamba jambo hili halina mbadala,imdhihirika kufuatia shambulio la kikatili lililofanywa na magaidi nchini Ufaransa.

Mwandishi: Mudhoon Loay
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Oummilkheri Hamidou