Maoni: Msaada wa kiutu ni uwekezaji wa siku zijazo
14 Oktoba 2020Mwanzoni mwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulidhani ungeweza kupeleka msaada wa kibinaadamu kwa watu milioni 168. Sasa ni watu milioni 250. Ongezeko hilo kubwa lililoshudhudiwa mwaka huu, limetokana na ugonjwa wa COVID-19. Janga la virusi vya corona na hatua zilizowekwa kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo, limesababisha mtikisiko wa kiuchumi ulimwenguni. Nchi zilizo kwenye mazingira magumu zaidi duniani zimeathirika vibaya. Hii imezidisha mizozo ya kibinaadamu iliyopo na imechochea mingine mipya.
Kwa mara ya kwanza tangu miaka ya 1990 umasikini uliokithiri utaongezeka. Umri wa watu kuishi utapungua. Idadi ya vifo vya kila mwaka vitokanavyo na virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na malaria inatarajiwa kuongezeka mara mbili. Pia inahofiwa kuongezeka mara mbili kwa idadi ya watu watakaokumbwa na njaa. Shule zimefungwa kwa wanafunzi milioni 500. Wasichana wengi ambao hawako shuleni, hawatorudi tena shule.
COVID-19 imeyaweka maendeleo katika hatari
Yote haya yatachochea mizozo, kukosekana kwa utulivu na kumiminika kwa wakimbizi. Madhara yake yatafika mbali na kudumu kwa muda mrefu. Na mzozo wa virusi vya corona bado haujamalizika. Umoja wa Mataifa unahitaji Dola bilioni 10 kwa ajili ya kupunguza athari zitokanazo na virusi hivyo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Hadi sasa, umepokea asilimia 28 tu ya fedha hizo.
Juhudi za haraka zinahitajika kuibadilisha hali hii. Bila kuchukua hatua sasa, mashirika ya kiutu yatalazimika kupunguza shughuli zake, hali itakayowagharimu mamilioni ya watu. Jumuia ya kimataifa inapaswa kuuzuia mzunguko huu mbaya. Kuwekeza sasa kutapunguza kiwango cha tatizo. Nchi zote zinapaswa kuonyesha mshikamano wa kimataifa na kutambua kuwa kutoa msaada wa kibinaadamu kunamaanisha kuwekeza katika siku zijazo kwa wale wenye mahitaji.
Kuwekeza katika siku zijazo
Huku Dola bilioni 2.9 tayari zikiwa zimepatikana kupitia mpango wa ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kukabiliana na masuala ya kiutu, misaada imewafikia mamilioni ya watu walioathirika, ikiwemo wakimbizi na wakimbizi wa ndani kwa kuwahamishia pesa; pia wametoa msaada zaidi kwa walionusurika na unyanyasaji wa kijinsia, kuanzisha vituo vya kunawa mikono na kutoa sabuni na huduma maalum kwa watoto na akina mama.
Pia wametoa barakoa milioni 78 kwa nchi zilizokuwa zinahitaji na kutoa elimu jinsi ya kuzuia COVID-19 kwa zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni kote.
Ujerumani ambayo ni rais wa sasa wa Baraza la Umoja wa Ulaya, hadi sasa imechangia Euro milioni 450 kama msaada wa ziada wa kukabiliana na janga la COVID-19. Nchi kama Ujerumani zinaweza kuchangia binafsi, lakini taasisi za kifedha za kimataifa zinanapaswa kuchangia zaidi. Ni muda wa kutumia taasisi zote zilizopo kwetu kuanzia Benki ya Dunia hadi Shirika la Fedha Duniani, IMF. Imefanyika kabla na inaweza kufanyika tena.
Msaada zaidi kwa nchi masikini
Wakati huo huo, tunaweza kusonga mbele na kuziangazia nchi zote ambazo msaada wa kimataifa unahitajika haraka. Baadae mwezi huu, Ujerumani, Denmark, Umoja wa Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa la uratibu wa misaada ya kiutu, OCHA, zitaandaa mkutano wa wafadhili wa masuala ya kiutu kwa ukanda wa Sahel ya Kati utakaozihusisha nchi za Mali, Burkina Faso na Niger, ambako janga la COVID-19 limezidisha tatizo la kibinaadamu mbali na lile liliopo sasa.
Tunaziomba serikali, taasisi za kifedha za kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia kuunga mkono juhudi hizi, kuzisaidia jamii maskini zaidi kupambana na virusi vya corona na kupunguza mtikisiko wa kiuchumi uliosababishwa na virusi hivyo. Ni kwa maslahi ya kila mtu kushughulikia matatizo haya sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Niels Annen ni Waziri wa Dola katika Ofisi ya Shirikisho ya Mambo ya Ujerumani. Mark Lowcock ni Mratibu wa Masuala ya Kibinaadamu na Msaada wa Dharura wa Umoja wa Mataifa.
(DW https://bit.ly/3k0Vtvc)