Wiki iliyopita ulimalizika kwa mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu uliofanyika Sharm Al Shaikh, nchini Misri. Huu ulikuwa mkutano wa kwanza kabisa wa aina yake baina ya pande hizi mbili, ambazo sio tu kwamba zinapakana kijiografia, lakini pia zina historia inayogusana kupitia ukoloni na wakati mwengine hata siasa za kilimwengu.
Pande zote mbili kwenye mkutano huo zilikiri kwamba mkutano huu ulikuwa umechelewa sana na kwamba lazima uendelee kuwapo mlahaka baina ya vyombo viwili hivi, huku pakipangwa mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa kukutana tena mjini Brussels, Ubelgiji.
Washiriki kwenye mjadala huu ni mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Ahmed Rajab, akiwa London, Uingereza. Mtaalamu wa siasa za Mashariki ya Kati, Dk. Harith Ghassany, akiwa Muscat, Oman na mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya Ghuba, Abdulfattah Mussa.