1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Juncker kuleta mabadiliko Ulaya?

Bernd Riegert22 Oktoba 2014

Wabunge wa Umoja wa Ulaya wameipitisha kamisheni mpya inayoundwa na makamishna 27 pamoja na mwenyekiti wao Jean-Claude Juncker. Bernd Riegert anatoa maoni yake juu ya viongozi hao wapya.

https://p.dw.com/p/1DZvq
Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Juncker (kulia) na spika wa bunge Martin Schulz (kushoto)
Picha: Reuters/Christian Hartmann

Jean-Claude Juncker huenda ndiye mwanasiasa wa Umoja wa Ulaya mwenye kufahamika zaidi. Kila mtu anamfahamu na yeye anamfahamu kila mtu. Amewahi kufikia makubaliano au kujadiliana na sehemu kubwa ya wanasiasa wenzake. Na yeye ndiye mtu mwenye uzoefu mwingi zaidi bungeni. Kwa miaka mingi alishikilia wadhifa wa mkuu wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro na hivyo anazifahamu sera za uchumi za Umoja wa Ulaya kwa undani kabisa. Juncker hawaogopi viongozi wenye mamlaka makubwa barani Ulaya. Iwe Kansela Angela Merkel wa Ujerumani au rais Francois Hollande wa Ufaransa - Juncker anazungumza na wote kwa uwazi. Hivyo ni vigezo vitakavyomsadia kiongozi huyo, anayekaribia kutimiza miaka 60, katika wadhifa wake huu mpya.

Kamisheni atakayoiongoza itashughulikia zaidi masuala ya uchumi. Umoja wa Ulaya bado uko kwenye mgogoro wa kiuchumi, licha ya kwamba maeneo mengine ya dunia yamefanikiwa kuishinda migogoro hiyo ya mwaka 2008 na 2009. Juncker anapinga hatua kali za kufunga mkaja lakini pia hataki nchi za Umoja wake zilimbikize madeni kupita kiasi. Na hii ni kawaida kwa mwanasiasa huyo. Daima anatafuta suluhu ya wastani. Anataka mataifa ya Ulaya yawekeze bila kuingia kwenye madeni.

Juncker atakiwa kuwa mshawishi

Alipoanza kampeni zake za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Juncker alionekana kama mtu asiye na msukumo. Lakini inaelekea kuwa alikusanya nguvu mpya miezi iliyopita na hilo litamsaidia kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kuliko kiongozi aliyemtangulia, Jose Manuel Barosso. Baadhi ya wanasiasa wa Brussels wanatumaini kwamba Juncker atakuwa kama Jacques Delors, mwenyekiti wa kamisheni aliyeleta mageuzi makubwa katika Umoja wa Ulaya miaka ya 1980. Lakini kibarua cha kuleta mabadiliko hakimwangukii Juncker pekee yake. Ana makamishna 27, kila mmoja akiiwakilisha nchi moja mwanachama.

Mwandishi wa DW mjini Brussels, Bernd Riegert
Mwandishi wa DW mjini Brussels, Bernd Riegert

Juncker itabidi ajifunze namna ya kuongoza kamisheni ya Umoja wa Ulaya yenye wafanyakazi 30,000. Na pia anatakiwa kuonyesha kwamba ana nguvu ya kubeba wajibu wa raia milioni 500 wa nchi mwanachama. Zamani Juncker alikuwa waziri mkuu wa Luxemburg, nchi yenye wakazi 500,000 tu!

Jukumu mojawapo la kiongozi huyo litakuwa kuwaelewesha watu umuhimu wa Umoja wa Ulaya. Ni jukumu linalohitajika sana kwani wengi wana mashaka iwapo kweli jumuiya hiyo ina umuhimu wowote. Mtihani mkubwa unaomsubiri Juncker ni swali iwapo ataweza kuishawishi Uingerezea kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya. Ni lazima azijibu nchi zote zenye mashaka na Umoja huo, si Uingereza pekee yake, bali hata Ufaransa, Italia na Hungary. Hapo Juncker atakuwa na wakati mgumu kwani serikali za Uingereza na Hungary hazikumuunga mkonopale alipogombea nafasi ya mwenyekiti wa kamisheni.

Mwandishi: Bernd Riegert

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman