MANILA: Mawaziri wa kigeni wa nchi za jumuiya ya ASEAN wakutana
30 Julai 2007Mawaziri wa kigeni wa jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, wameyapongeza makubaliano ya kuunda shirika la kikanda litaloshughulikia haki za binadamu.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo kwenye mkutano wao wa mwaka mjini Manila nchini Ufilipino. Hata hivyo jumuiya hiyo imeendela kuukosoa utawala wa kijeshi wa Myanmar.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufilipino, Alberto Romulo, amesema makubaliano hayo ni ushindi mkubwa kwa watetezi wa haki za binadamu katika eneo hilo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa mjini Manila, rais wa Ufilipino, Gloria Arroyo, amesema jumuiya ya ASEAN ina lengo moja la kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa. Aidha rais Arroyo amesema, ´Nafasi ya kiuchumi na usalama wa pamoja kwa eneo hili ni lengo letu la msingi. Tangazo letu la katiba ya jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ni ushahidi wa kujitolea kwetu kuwa na kanda moja iliyoungana.´
Nchi 10 za jumuiya ya ASEAN zimekubaliana juu ya pendekezo la katiba ya jumuiya hiyo kwenye mkutano wa leo mjini Manila.
Maswala mengine yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni vita dhidi ya ugaidi, kuunda shirika la kikanda litakalokabiliana na majanga asili na shirika litakalohakikisha vinu vya nyukilia katika eneo hilo havitumiwi kutengeneza silaha za kinyuklia.