City kuchuana na Inter katika fainali ya Ligi ya Mabingwa
10 Juni 2023Vijana wa Pep Guardiola tayari wameshinda taji la Ligi Kuu ya Premia na Kombe la FA.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa Manchester City kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, na walifungwa na Chelsea msimu wa mwaka 2020-21.
Guardiola anasaka taji lake la Ulaya kwa mara ya kwanza tangu alipofanya hivyo mnamo mwaka 2011 akiwa mkufunzi wa Barcelona, ambapo pia alishinda mataji matatu miaka miwili kabla ya hapo.
Manchester United ndio klabu pekee ya Uingereza iliyowahi kushinda mataji matatu kwa msimu mmoja. Mnamo msimu wa mwaka 1998-99, Mashetani hao wekundu walishinda taji la Ligi Kuu ya Premia, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Inter Milan haijapewa nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo, japo ina historia nzuri ya Ulaya tofauti na City, kwani wamewahi kushinda Ligi ya mabingwa barani Ulaya mara tatu.
Mara ya mwisho kushinda taji hilo ilikuwa mnamo mwaka 2010, wakati huo ikitiwa makali na Jose Mourinho.