Mamlaka Msumbiji zatishia kutumia jeshi kudhibiti maandamano
7 Novemba 2024Maelfu ya watu wameingia mitaani tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo. Ushindi huo unarefusha utawala wa Frelimo ambacho kimekuwa madarakani nchini Msumbiji kwa miaka 49.
Matokeo hayo yamepingwa vikali na upande wa upinzani ambao umesema unapanga kuitisha maandamano makubwa leo kwenye mji mkuu Maputo. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema hapo jana kwamba takribani watu 20 wameuawa na mamia wengine wamejeruhiwa na kukamatwa tangu kuanza kwa maandamano hayo.
Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji Cristóvão Chume ametishia kuwatuma wanajeshi mitaani kuzima maandamano yanayoendelea akisema yamekuwa ni jaribio la kuipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.
Amesema iwapo machafuko yataendelea wanajeshi watachukua jukumu la polisi kulinda kile amekitaja kuwa "maslahi ya taifa".