Mamlaka Misri zashutumiwa kuvunja haki za watumiaji mitandao
18 Agosti 2020Taarifa iliyotolewa Jumatatu na shirika hilo la haki za binaadamu inasema kuwa vyombo vya usalama vimeshawatia nguvuni watu 15, miongoni mwao akiwa msichana wa miaka 17 ambaye alituma vidio kuhusu kupigwa na kubakwa.
Serikali imewafungulia watu hao mashitaka, ambayo Human Rights Watch inasema ni ya ovyo, kama vile kuvunja maadili ya kijamii na kuhujumu misingi ya kifamilia.
Soma zaidi Sisi atishia kuivamia Libya kijeshi
Watatu katika hao waliokamatwa ni wanaume wanaoshukiwa kuwasaidia wanawake wawili. Wanawake wengi walikamatwa kwa kile serikali inachosema ni vidio zisizo za heshima kwenye mitandao ya kijamii, hasa kwenye mtandao wa TikTok.
Hata hivyo, Human Rights Watch inasema kwenye vidio na picha nyingi, wanawake hao wanaonekana wakiwa wamejitanda mwili mzima huku wakiimba ama kucheza. Wengi wao wana wafuasi weni kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakipindukia mamilioni.
"Kuwakamata wanawake na wasichana kwa sababu za ovyo kama huko tu kutuma vidio na picha zao wenyewe kwenye mitandao ya kijamii ni ubaguzi na kunavunja moja kwa moja haki yao ya uhuru wa kujieleza,” amesema Rothna Begum, mtafiti mkuu wa haki za wanawake kwenye shirika hilo la Human Rights Watch, aliyeongeza kwamba "kufuatilia tabia za wanawake mitandaoni ni juhudi mpya za kudhibiti uwezo wao wa kujieleza hadharani.”
Makali ya sheria ya uhalifu wa mitandaoni
Mashitaka haya yanaonekana kuwa matumizi ya kwanza ya kesi za maadili chini ya sheria ya uhalifu wa mitandaoni ya mwaka 2018. Taarifa kutoka ofisi ya mwendesha mashitaka zinadai kuwa kesi zilifunguliwa baada ya baadhi ya watumiaji wa mitandao kuwasilisha malalamiko yao kupitia mtandao wa Facebook wa ofisi hiyo.
Soma zaidi Misri: Polisi wapambana na waandamanaji
Tayari washukiwa wawili wa kike na watatu wanaume wameshahukumiwa vifungo vya miaka miwili kila mmoja na wanawake wengine wawili wakihukumiwa kifungo cha miaka mitatu kila mmoja kwenye kesi tafauti.
Wanawake saba na msichana mmoja waliobakia wanaendelea na kesi mahakamani. Kitengo cha Maadili cha Polisi kilicho chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kimehusika na kesi kadhaa za aina hii.
Mtu wa kwanza kukamatwa mnamo tarehe 21 Aprili alikuwa Hanin Hossam, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 20 na mwenye malaki ya wafuasi katika mitandao ya TikTok na Instagram.
Ushahidi mkubwa wa mwendesha mashitaka dhid ya Hanin ni vidio aliyoituma kwenye TikTok, akiwaalika wafuasi wake wa kike kutumia jukwaa jengine la vidio mitandaoni la Likee, akiwaambia kuwa wanaweza kupata fedha kwa kurikodi vidio za mubashara kwenye mtandao huo ambazo zinakuwa na watazamaji wengi zaidi.
Soma zaidi Misri: Kura ya maoni kumruhusu el Sissi kutawala hadi 2030
Wengine walikamatwa kufuatia kauli ya tarehe 2 Mei ya ofisi ya mwendesha mashitaka ambayo ilisema "nguvu za uovu” zilikuwa zinatumia vibaya "fursa ya mitandao ya kijamii kuharibu jamii, kuporomosha maadili na misingi yake.”
Mnamo tarehe 11 Juni, waendesha mashitaka waliwasilisha mashitaka dhidi ya Hanin kwenye mahakama ya Uhalifu wa Uchumi mjini Cairo, ambayo pia hushughulikia kesi za uhalifu wa mitandao. Kesi waliyomfungulia ni "kuhujumu maadili na misingi ya kifamilia.”
Nini hasa kuhujumu maadili ya familia?
Kwenye kesi hiyo hiyo pia, waendesha mashitaka wanamshitaki Mawadda al-Adham, mwanamke mwenye umri wa miaka 22, na pia na wanaume watatu ambao wanasema waliwasaidia Hanin na Mawadda. Mawadda aliongezewa mashitaka ya kuchapisha vidio chafu na kutengeneza na kusimamia tovuti kwa malengo hayo hayo ya kuhujumu maadili ya kifamilia.
Soma pia Bunge la Misri kuidhinisha mageuzi ya katiba
Mnamo Juni 27, mahakama hiyo iliwatia hatiani Hanin na Mawadda na kuwafunga miaka miwili jela na faini ya paundi 300,000 za Kimisri kila mmoja - sawa na dola 19,000 za Kimarekani. Hukumu pia ilitolewa dhidi ya wanaume waliotiwa hatiani kwa kutengeneza na kusimamia tovuti bila kibali.
Shirika la Human Rights Watch limezitaka mamlaka nchini Misri kuwaachia huru wote bila masharti na kwamba ziwache mara moja kuingilia uhuru wa wanawake na wasichana kujieleza kutumia mitandao ya kijamii na kuheshimu sheria za kimataifa zinazowalinda watoto, kwani mmoja wa waliofungwa kwenye kampeni hii ya serikali ni msichana mwenye umri wa miaka 17.
Chanzo: HRW