UNICEF: watoto milioni 500 wanakabiliwa na kitisho
24 Novemba 2015Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto - UNICEF linalosema kuwa mamia ya mamilioni ya watoto wanakabiliwa na kitisho cha athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Ripoti ya UNICEF imesema karibu watoto milioni 530 wanaishi katika maeneo yenye hatari kubwa ya kutokea mafuriko, mengi yakiwa barani Asia, wakiwemo watoto milioni 300 katika mataifa ambayo nusu au zaidi ya idadi ya watu ni maskini.
Ripoti hiyo iliyotolewa kabla ya kuanza mazungumzo ya wiki mbili ya mabadiliko ya tabia nchi mjini Paris, Ufaransa, imeongeza kuwa karibu watoto milioni 160 wanaishi katika sehemu za ulimwengu ambazo zinakumbwa na ukame, zaidi ya nusu yao barani Afrika, na zaidi ya milioni 115 wanaishi katika maeneo yenye kitisho kikubwa kabisa cha kutokea vimbunga.
Mataifa tayari yameahidi kujaribu kupunguza kiwango cha joto hadi nyuzi joto mbili, ili kuepusha athari zenye uharibifu mkubwa katika siku za usoni za kuendelea kuharibika hali ya hewa na kupungua viwango vya maji baharini.
Lakini mipango ya kitaifa ya kukabiliana na gesi zinazochafua mazingira na kuongeza kiwango cha joto, iliyowekwa kabla ya mkutano wa kilele wa Paris, hazitoshi kutimiza lengo hilo.
Ripoti ya shirika hilo la umoja wa Mataifa la kuwashughulikia watoto imesema makadirio ya kisayansi yanaonyesha kuwa “ikiwa hatua zitachukuliwa kwa kiwango kikubwa, kutakuwa na nafasi kubwa ya kuwaokoa watoto dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabia nchi”.
Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Anthony Lake anasema lazima pia tushughulikie athari za gesi ya kaboni iliyo hewani kwa sasa kwa sababu tayari watoto wanakumbwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
UNICEF inasema hali mbaya ya hewa inawaumiza watoto kwa kuongeza utapiamlo na kuenea kwa maradhi makuu yanayouwa, yakiwemo Malaria na kuharisha.
Mtoto asiyepata maji ya kutosha na mazingira safi kabla ya mgogoro ataathirika zaidi na mafuriko, ukame au kimbunga kikali, asiwe na nafasi kubwa ya kupona haraka.
UNICEF inatoa wito kwa mahitaji ya watu wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo watoto, kupewa kipaumbele katika juhudi za kuyakabili mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na hatua za kuwalinda wale wanaoachwa bila makazi kutokana na majanga au mazingira yasiyokalika.
Nakala ya rasimu ya muafaka unaotarajiwa kufikiwa na wajumbe wa mkutano wa Paris, unaofahamika kama COP21, inasema serikali zinapaswa kuheshimu na kuzingatia mahitaji ya watoto, miongoni mwa makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu, wakati zikiyakabili mabadiliko ya tabia nchi.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Caro Robi