Mamilioni kukumbwa na njaa kutokana na COVID-19
2 Julai 2020Mtendaji Mkuu wa WFP, David Beasley, amesema makabiliano ya vita dhidi ya virusi vya corona yameanza kuhama kutoka kwa mataifa tajiri kuelekea kwenye mataifa masikini, na kuongeza kwamba hadi utakapofikia wakati wa kupatikana kinga, chakula kitasalia kuwa kinga bora dhidi ya mikasa ya vurugu duniani.
Taarifa zaidi: UNICEF: mamilioni ya watoto kukabiliwa njaa Yemen
Amesema pasipo upatikanaji wa chakula cha kutosha, ulimwengu utashuhudia hali ya vurugu miongoni mwa jamii na maandamano, kuongezeka kwa uhamiaji, kuongezeka migogoro na kuongezeka kwa utapiamlo kutokana na lishe duni, kwa miongoni mwa idadi ya watu ambao awali waliweza kukingwa dhidi ya njaa.
Juhudi za kutoa msaada wa chakula zaongezwa
Kwa shabaha ya kukabiliana na wimbi hilo la njaa, WFP ipo katika jitihada ya kufanikisha msaada mkubwa kabisa wa kiutu wa kihistoria, wenye lengo la kunusuru maisha ya watu milioni 138, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na rekodi ya awali ya 2019 ya watu milioni 97. Shirika hilo limesema mchango madhubuti unahitajika ili kuwezesha majukumu yake katika mataifa 83, kutoa msaada wa chakula katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kuzisaida serikali katika jitihada zao za kukabiliana na kusambaa kwa COVID-19.
Taarifa zaidi: UN yasema watu milioni 820 wanakabiliwa na kitisho cha njaa
Kwa mujibu wa WFP, idadi ya watu wenye kukabiliwa na njaa inaweza kufikia watu milioni 270, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa 2020. Ikiwa ni ongezeko la asilimia 82 kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya corona. Athari za janga hilo limejidhihirisha zaidi katika mataifa ya Amerika ya Kusini ambako kumebainika kiwango kikubwa cha ongezeko la idadi ya watu wenye kuhitaji msaada wa chakula, wakiwemo miongoni mwa wakazi wa mijini wa kipato kidogo na cha kati, ambapo inaonekana wanaburuzwa kuelekea katika kupoteza ajira zao na kushuka kiwango cha ajira katika shughuli wanazofanya.
Hali tete Afrika
Hali ya njaa pia imejidhihirisha katika mataifa ya Magharibi na ya Kati ya Afrika, ambako kuna ongezeko la kasi la asilimia 135 la uhaba wa chakula, yakiwemo ya Afrika ya Kusini, ambapo kuna mashaka ya ongezeko la asilimia 90. Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona yanazidi kupanda wakati hifadhi ya chakula kwa baadhi ya maeneo tayari imekwishapungua.
Katika kipindi hiki, wakulima wengi wanasubiri mazao kutokana na mavuno mapya. Vimbunga na mvua kubwa viko njiani, huku rekodi za uvamizi wa nzige katika eneo la Afrika Mashariki na kuzuka kwa migogoro vinaongeza changamoto iliyokuwepo ya hali ya njaa ya ulimwengu.
Kutokana na hali hiyo, Mtendaji Mkuu wa WFP, David Beasley anasema mgogoro huo ambao haujawahi kushuhudiwa unahitaji kushughulikiwa kwa namna isiyo ya kawaida. Na ameonya kwamba endapo hakutachukuliwa hatua za haraka na mahususi kwa virusi hivyo vilivyotapakaa, matokeo yake yatakuwa kupotea kwa maisha katika kiwango kisicho kifani, na juhudi za kukabiliana na wimbi la janga la njaa litakuwa si lolote si chochote.
Changamoto mpya inahitaji ongezeko kubwa la matumizi ya fedha taslimu, katika usafirishaji pesa. Zaidi ya nusu ya mipango ya WFP katika kukabiliana na kitisho cha njaa, kitafanyika kwa kutoa pesa na hundi ambazo zitawezesha wakazi wa mijini kununua vyakula wanavyohitaji masokoni, ambavyo vinatasaidia uchumi wa jamii katika maeneo husika.
Chanzo: AP