1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia warejea nyumbani katika ubadilishaji wafungwa Yemen

15 Oktoba 2020

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na waasi wa kihouthi wa Yemen wamekubaliana kubadilishana wafungwa 1,081 na raia wa Saudia 15, katika ubadilishaji mkubwa kutokea tangu mwanzo wa mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/3jzEs
Jemen Sanaa | Huthi Rebellen lassen mehrere hundert Insassen frei
Picha: picture-alliance/AA/M. Hamoud

Ndege zilizobeba wafungwa waliobadilishwa na pande hasimu nchini Yemen zilipaa kutoka viwanja vitatu tofauti, katika operesheni ya kuwarejesha nyumbani wanaume wapatao 1,000 waliotekwa katika mapigano. 

Ubadilishanaji huo ni ishara ya nadra ya hatua katika mchakato wa kumaliza mzozo uliyozuka miaka sita iliyopita nchini Yemen, ambako Wahouthi wanaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya upande kaskazini licha ya uingiliaji wa Saudi Arabia na washirika wake tangu mwaka 2015.

Duru zimesema kuwa ndege mbili zilibeba wanachama wa muungano unaongozwa na Saudia walioachiliwa kutoka kizuizini, ziliondoka kutoka uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi. 

Ndege moja iliyokuwa imebeba wafungwa wa Saudia na Sudan ilielekea Saudi Arabia huku nyengine ikielekea katika uwanja wa ndege unaodhibitiwa na serikali wa Sayoun katika mkoa wa Hadramount.

Yemen Huthi Kämpfer
Wapiganaji wa kihuthiPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Taarifa zinaashiria kuwa ndege iliyobeba Wahouthi waliotolewa  kifungoni na muungano huo iliondoka katika uwanja wa ndege wa Sayoun na ndege ya pili iliwasili kutoka uwanja wa Abha nchini Saudi Arabia.

Kupitia ukurasa wa twitter kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu ICRC imesema jumla ya ndege tano zimepaa kutoka viwanja vya ndege vya Sayoun, Sanaa na Abha.  SomaYemen Kusini waachana na tangazo la kujitawala ili kusaka amani

Akizungumza na Reuters mkurugenzi wa kanda wa shirika la Msalaba mwekundu Fabrizio Carboni amesema operesheni hiyo inayoendelea inamaana kubwa sana kwa familia nyingi, licha ya kuwa ubadilishanaji wa wafungwa unaendelea wakati mzozo bado ungalipo.

Jemen Konflikt Saudi Arabien
Wanajeshi wa Saudia Picha: Getty Images/A. Al-Qadry

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa vita hivyo vimesabaisha vifo vya zaidi wa watu laki moja, na kusabadisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu duniani.

"Ningependa tu kutoa shukrani zangu za dhati kwa utukufu wake Sultan bin Haitham kwa kupanga kuachiliwa kwetu na mamlaka huko Sanaa, nina shukuru sana na nina furaha sana leo."Sandra Loli ni mmoja wa mateka aliyeachiliwa huru

Mikael Gidada vile amesema "Nilikuwa naishi na kufanya kazi Yemen na nilikuwa gerezani kwa miaka 2 na siku 199 na kuna kipindi cha miezi 6 nilikuwa katika kifungo cha peke yangu. Ilikuwa kuzimu, hali ilikuwa mbaya sana,  Nashukuru Sultan Haitham kwa msaada wake kututoa Sanaa. 

Kamati ya ICRC, inayohudumu kama mpatanishi kati ya pande zote, ilipeleka zaidi ya wafanyikazi 70 ambao walifanya ukaguzi wa matibabu pamoja na kutoa vifaa vya kinga na hatua zingine za ulinzi dhidi ya hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. Vile vile wafanyikazi hao walifanya mahojiano ya moja kwa moja na wafungwa ili kuhakikisha walitaka kurudishwa nyumbani.