Mamia wakimbia eneo la mapigano nchini Syria
12 Februari 2019Kulipombazuka leo Jumanne viunga vya eneo la Baghouz vilikuwa vimetapakaa mabaki ya mizinga, chupa tupu za maji , nguo zilizotelekezwa na mizoga ya mbwa iliyoanza kuoza .
Mamia ya watu waliondoka kutoka eneo la mapigano la Baghouz jana usiku na tayari wameanza kupokelewa katika vituo vya kusajili raia wanaokimbia vita nchini Syria.
Baghouz, kijiji kilichopo mashariki ya ukingo wa mto Euphrates kwenye mpaka kati ya Syria na Iraq ndiyo eneo la mwisho linalodhibitiwa na kundi la dola la kiislam katika ukanda ambao muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani unaendesha operesheni yake.
Baada ya kusimama kwa muda wa wiki moja ili kupisha raia kuondoka kutoka eneo la mapigano, jumamosi iliyopita jeshi la wakurdi nchini Syria SDF lilitangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kuchukua udhibiti wa eneo linalokaliwa na wapiganaji wa IS.
Ushindi unapatikana pole pole
Msemaji wa vikosi vya Marekani Sean Ryan amesema wamekuwa wakikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa kundi la jihad IS ambao wanatekeleza mashumbulio ya kuvizia na kwamba wamekuwa wakipata mafanikio madogo na ya pole pole.
Kulingana na msemaji wa wapiganaji wa jeshi la wakurdi Mostefa Bali mapigano makali yanatarajiwa leo jumanne baada ya mamia ya raia kuondoka kutoka eneo la mapambano usiku wa kuamkia leo.
Vikisadiwa kwa ndege za kivita pamoja na silaha nyingine nzito nzito chini ya muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani, vikosi vya wakurdi vimefanikiwa kusonga mbele katika eneo la kilometa nne za mraba ambalo lilikuwa likidhibitiwa na wapiganaji wa IS.
Mashambulizi ya anga yanaua raia
Hata hivyo shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria limesema sehemu kubwa ya waliondoka kutoka eneo la mapigano ni raia wa kigeni zaidi kutoka mataifa ya Ufaransa na Ujerumani.
Hapo jana shirika hilo lilisema mashambulizi ya anga yanayaongozwa na muungano wa kijeshi wa Marekani yaliwaua raia 16.
Siku ya jumamosi iliyopita msemaji wa jeshi la wakurdi alisema wanakadiria kuna wapiganaji zaidi ya 600 wa IS ambao wamesalia kwenye kijiji cha Baghouz lakini hakuna uwezekano kwamba kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi yupo kwenye eneo hilo.
Kundi la dola la kiislam lilitangaza kuanzisha utawala wa kihalifa nchini Syria na Iraq mnamo mwaka 2014 lakini operesheni kadhaa za kijeshi zimefanikiwa kupunguza nguvu ya kundi hilo hadi kusalia na eneo dogo kabisa wanalolidhibiti.
Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu