1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo muhimu yanayojenga uhusiano wa India na Urusi

10 Julai 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi yuko nchini Urusi tangu Jumatatu kwa ziara inayolenga kuimarisha uhusiano kati yao, ushirikiano kati ya mataifa hayo umeundwa chini misingi ya kihistoria na masuala ya kimkakati.

https://p.dw.com/p/4i4Ct
Diplomasia |  Narendra Modi na Vladimir Putin
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiwa na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/TASS/dpa/picture alliance

Katika wakati mahusiano baina ya nchi hizo mbili yanapitia vizingizi hasa tangu kuzuka vita vya Ukraine, maswali yanaulizwa juu ya kile Putin na Modi wanalenga kukifanikisha? 

Katika miaka ya hivi karibuni, India imekuwa moja ya mwagizaji mkubwa wa mafuta na makaa ya mawe ya Urusi, ikitumia vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Urusi na mataifa ya magharibi ili kupata bei nafuu.

Hatua hii ya kimkakati sio tu imelinda mahitaji ya nishati ya India bali pia imethibitisha uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili.

Licha yaukosoaji kutoka upande wa magharibi unaosema ununuzi huu wa nishati ya Urusi ni sawa na kuunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja vitendo vya kijeshi vya Urusi, India imedumisha msimamo wake, ikisisitiza umuhimu wa usalama wa nishati na urafiki wa muda mrefu na Urusi.

Soma pia:Waziri Mkuu wa India Modi kufanya mazungumzo na Rais Putin

Kulingana na tathmini iliyochapishwa na Dkt Aleksei Zakharov, mtafiti wa sera za kigeni za India katika Taasisi ya Uhusiano ya Kimataifa ya Ufaransa, ''New Delhi imeonyesha mtazamo tofauti wa kukabiliana na mzozo wa Urusi na Ukraine, ikikaa katika uhusiano mzuri na Moscow na vilevile nchi za magharibi" 

Zakharov alifafanua zaidi  juu ya "changamoto za kimuundo" ambazo alisema "zinaonekana bado kuzuia pande hizo mbili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, na kuongeza kuwa ushirikiano wa ulinzi kati ya Urusi na India kwa sasa "uko katika hali ya sintofahamu," ikichangiwa na vita vya Ukraine.Vikwazo vimeitatiza sekta ya silaha ya Urusi.

Mbali ya suala la nishati Urusi pia imekuwa msambazaji mkuu wa vifaa vya kijeshi kwa India, uhusiano ambao umekuwa msingi wa mkakati wa ulinzi wa India lakini umeleta mashaka miongoni mwa washirika wa India upande wa madola ya magharibi. 

Changamoto kati ya mataifa hayo

Hata hivyo, kama ushirikiano wowote wa kudumu, umekabiliwa na changamoto zake, huku India ikikumbana na vikwazo katika baadhi ya mikataba ya ulinzi. Changamoto hizi, hata hivyo, hazijaizuia India kufanya biashara na Urusi au kushusha thamani na umuhimu ya Uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

Sera ya kigeni ya India inasisitiza usawa kati ya mataifa yote.Sera hii inalenga kuimarisha uhusiano na nchi za Magharibi huku ikidumisha uhusiano thabiti na Urusi, wakati wote ikitetea amani na mazungumzo ili kusuluhisha migogoro.

Usawa huu unaonyesha kujitolea kwa India kwa mpangilio wa ulimwengu wa pande nyingi, ambapo diplomasia na mazungumzo huchukua nafasi ya kwanza juu ya mgawanyiko. Hata hivyo kuna matundu yanayoonekana wazi kwenye usuhuba huu. 

Licha ya India kusalia kuwa nchi inayoongoza kwa ununuzi wa silaha kutoka Moscow kati ya 2017 na 2022, sehemu ya Urusi ya mauzo ya nje ya ulinzi kwenda nchi ya  ilishuka kutoka 65% hadi 36% katika kipindi hicho, data ta taasisi ya utafiti wa masuala ya amani, SIPRI ilionyesha.

Mazungumzo yamekwama baina ya Ukraine na Urusi

Soma pia:Marekani yamtaka Modi kusisitiza juu ya uadilifu wa Ukraine

Wasambazaji wa silaha wa Ufaransa na Ujerumani wamenufaika kutokana na mabadiliko ya mkakati wa New Delhi, huku kukiwa na kutosita miongoni mwa watunga sera wa India kuvunja vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kwa kutia saini mikataba mipya na Kremlin.

 Ziara ya wiki hii ya  Waziri Mkuu Narendra Modi mjiniMoscow inadhihirisha kwa mara nyingine umuhimu wa ushirikiano wa India na Urusi.

Ni fursa sio tu ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara lakini pia kuchunguza njia mpya za ushirikiano, kupitia miradi kadhaa kama vile upanuzi wa Ukanda wa Kimataifa wa Usafiri wa Kaskazini-Kusini na maendeleo ya Ukanda wa Bahari wa Chennai-Vladivostok.

Mipango hii inajumuisha ahadi ya kutanua biashara na kuyaunganisha mataifa hayo mawili na kutangaza enzi mpya ya ushirikiano.

Uhusiano kati ya India na Urusi ni ushuhuda wa hali ya ushirikiano wa kimkakati katika ulimwengu unaobadilika haraka. Ni uhusiano ambao unahusu uhusiano wa kihistoria kama vile matarajio ya siku zijazo, unaozingatia manufaa na heshima ya pande zote.