1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yatangaza serikali mpya yenye maafisa wa kijeshi

Sylvia Mwehozi
12 Juni 2021

Tangazo hilo linakuja baada ya Kanali Assimi Goita, ambaye aliongoza mapinduzi mwezi uliopita, kuteuliwa kama rais wa mpito wiki hii na kisha kumteua kiongozi wa kiraia kama waziri wake mkuu

https://p.dw.com/p/3unGd
Mali Oberst Assimi Goita, Anführer der malischen Militärjunta
Picha: Annie Risemberg/AFP/Getty Images

Goita alikuwa ameongoza mapinduzi ya mwezi Agosti, wakati yeye na maafisa wengine wa jeshi walipomwondoa mamlakani rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita baada ya maandamano ya wiki kadhaa juu ya ufisadi na mzozo wa muda mrefu wa wanajihadi.

Baada ya Jumuiya ya Afrika Magharibi ya ECOWAS kuweka vikwazo, mamlaka ya kijeshi ilikabidhi mamlaka kwa serikali ya mpito inayoongozwa na raia, lakini Goita aliwapindua tena viongozi hao mnamo Mei 24. Ufaransa yenye wanajeshi wake nchini humo imesimamisha ushirikiano wa kijeshi na Mali

Mwezi uliopita wanajeshi nchini Mali walimkamata rais na waziri mkuu wa serikali ya mpito iliyoundwa baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi ya Agosti mwaka uliopita.

Maafisa wa jeshi waliwaachia viongozi hao siku kadhaa baadaye, lakini walitangaza kuwavua madaraka yao katika mkasa uliozusha lawama kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.

Nyuma ya yote hayo akajitokeza Kanali Goita, afisa kijana wa jeshi na kamanda wa zamani wa operesheni maalum za jeshi la Mali ambaye tangu kuingia kwake katika uga wa siasa za nchi hiyo amesalia kuwa fumbo. Ni wachache sana wanaofahamu azma ya mwanajeshi huyo.

Mali Oberst Assimi Goita, neuer Übergangspräsident
Kanali Assimi Goita aliyepindua serikali za kiraia MaliPicha: Xinhua/imago images

Tangu mwanzo Goita hakuwa mtu anayefahamika kabisa hadi alipoingia kwenye uwanja wa siasa za Mali pale alipoongoza mapinduzi ya Agosti 18.

Mapinduzi hayo yalimwondoa madarakani ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia Ibrahim Boubacar Keita, ambaye utawala wake ulikabiliwa na maandamano ya wiki kadhaa kwa tuhuma za kugubikwa na rushwa na kushindwa kudhibiti uasi wa itikadi kali nchini Mali.

Goita aliyekuwa na umri wa miaka 37 wakati huo alisema baada ya mapinduzi hayo "Mali haikuwa na sababu ya kufanya tena makosa".

Afisa huyo ambaye huzungumza kwa nadra ni mtoto wa mkuu wa zamani wa polisi ya jeshi la Mali na alisoma kwenye shule ya jeshi la nchi hiyo. Mnamo mwaka 2002,  alikwenda kaskazini mwa Mali kwa ajili ya mafunzo na baadaye alitumia muda mrefu kwenye miji ya kaskazini ya  Gao, Kidal, Timbuktu, Menaka na Tessalit.

Goita pia alishuhudia uasi wa jamii ya kabila la Tuareg wa mwaka 2012 waliokuwa wakidai uhuru wa eneo la kaskazini mwa Mali.

Uasi huo uligeuka na kuwa vuguvugu lililodhibitiwa na wanamgambo wa itikadi kali ambalo tangu wakati huo limekuwa likiihangaisha Mali kwa mashambulizi ya kuvizia yaliyowauwa maelfu ya raia na kuwalazimisha wengine kuyakimbia makaazi yao.