Malala na Satyarthi washinda Tuzo ya Amani ya Nobel
10 Oktoba 2014kutokana na mchango wao mkubwa kwenye masuala ya haki za kielimu na kijamii kwenye eneo hilo la kusini mwa Asia.
Wanatokea kwenye nchi mbili tafauti ambazo hadi katikati ya karne iliyopita zilikuwa nchi moja iliyojuilikana kama Bara Hindi. Wanaunganishwa na dhamira moja ya kuona watoto wa eneo hilo na ulimwenguni kote wanapatiwa haki zao za kimsingi zikiwemo za kielimu. Hivi ndivyo, mjumbe wa Kamati ya Nobel, Thobjorn Jagland, alivyomuelezea Malala, ambaye miaka miwili iliyopita alipigwa risasi ya kichwa na wanamgambo wa Taliban, kwa kupigania kwake haki za wasichana kwenda shule: "Licha ya ujana wake, Malala Yousafzai tayari ameshapambana kwa miaka kadhaa kwa ajili ya haki za wasichana kwenye elimu na ameonesha kwa mifano kwamba watoto na vijana pia wanaweza kuchangia kwenye kuzifanya hali zao kuwa bora".
Mshindi mwenzake wa nishani hiyo yenye thamani ya dola milioni 1.1 na ambayo itakabidhiwa kwao tarehe 10 Disemba mjini Oslo, Norway, Kailash Satyarthi, anafahamika kwa harakati zake za kupigania haki za watoto nchini India, taifa la pili kwa kuwa na idadi ya watu wengi duniani. Akiwa na umri wa miaka 60 sasa, Satyarthi amekuwa akidumisha itikadi ya Mahatma Gandhi ya kupigania mabadiliko kwa njia za amani. Tena huyu hapa mkuu wa kamati ya Nobel, Thobjorn Jagland "Akionesha ujasiri wa hali ya juu kabisa, Kailash Satyarthi anadumisha mila ya Gandhi, ameitisha maandamano ya aina mbalimbali, yote kwa njia za amani, akijikita kwenye kupingana na unyanyasaji dhidi ya watoto kwa maslahi ya kifedha. Amechangia kwenye kuasisiwa na kupitishwa maazimio muhimu ya kimataifa juu ya haki za watoto".
Jagland amesema Kamati yake imezingatia muhimu wa muumini mmoja wa madhehebu ya Kihindu na mwengine Muislamu, mmoja raia wa India na mwengine wa Pakistan, kuungana kwenye mapambano yao ya pamoja kwa ajili ya elimu na dhini ya siasa kali. Malala mwenye umri wa miaka 17 anakuwa mshindi mdogo kabisa kwenye historia ya nishani hiyo ya amani.
Baadhi ya wachambuzi wanasema tunzo hii ya amani kwa Malala inaweza kumuongezea vitisho vya kushambuliwa tena na Taliban. Mwaka huu, Malala alitembelea Nigeria ambako alimshinikiza Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kukutana kwa mara ya kwanza na wazazi wa wasichana waliotekwa na kundi la Boko Haram.
Orodha ya wagombea wa Tunzo hiyo ya Amani ya Nobel mwaka huu ilikuwa kubwa kuliko mara nyengine zote, wakiwemo watu 231 na mashirika 47 yaliyoteuliwa kuwania nishani hiyo ya juu kabisa kimataifa. Miongoni mwao alikuwa Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, na pia mvujisha siri wa Marekani, Edward Snowden, gazeti huru la kila siku nchini Urusi, Novaya Gazeta, na mwanafizikia wa Kongo, Denis Mukwege.
Hata hivyo, uteuzi unaofanywa na kamati ya wajumbe watano wa Nobel kuna wakati umekuwa ukizua utata, mathalani ule wa mwaka 2009 ambao ulimtunuku Rais Barack Obama wa Marekani nishani ya amani, akiwa ndio kwanza ametimu mwaka mmoja madarakani.
Uungaji mkono wake kwa mashambulizi ya ndege zisizo rubani na pia mauaji ya raia wa nchi yake na nchi nyengine wanaoshukiwa kwa ugaidi, kumewafanya watu kadhaa duniani kutaka Kamati ya Nobel imnyang'anye tunzo hiyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf