Makundi yanayozozana Burundi sharti yazungumze: Mjumbe wa UN
10 Agosti 2018Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi ameliomba Baraza la Usalama kuyasihi makundi yote yanayozozana kushiriki katika mazungumzo mapya yanayolenga kusaidia kumaliza mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Michel Kafando ameliambia baraza hilo kuwa tangazo la Rais Pierre Nkurunziza la mwezi Juni kuwa hatogombea kwa muhula mwingine na atamuunga mkono mshindi wa uchaguzi wa 2020 unatoa fursa nzuri ya kupiga hatua katika kufikia suluhisho la mwisho la suala la Burundi.
Kafando amesema Rais wa Uganda Yoweri Museveni na rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye ndiye mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya Burundi, wamedhamiria kuanzisha upya mazungumzo kati ya serikali na upinzani haraka iwezekanavyo.
Mazungumzo hayo yanapangwa kuandaliwa Entebbe, Uganda au Arusha, Tanzania. Tangu kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu katiba mpya mwezi uliopita, na kutolewa tangazo hilo la rais, Kafando amesema hali nchini humo ni tulivu isipokuwa tu maandamano kadhaa kutoka upinzani.