1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yakaribia kupatiwa msaada mwingine

Admin.WagnerD11 Agosti 2015

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imesema kwamba Ugiriki kimsingi imefikia makubaliano na wakopeshaji wake wa kimataifa juu ya kupatiwa mkopo mwingine kwa ajili ya kuiokoa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1GDZh
Griechenland / Alexis Tsipras im Parlament
Picha: Reuters

Serikali ya Ugiriki imeeleza kuwa baada ya mazungumzo yaliyofanyika hadi alfajiri ya leo mjini Athens, makubaliano yamefikiwa kimsingi baina ya nchi hiyo na wakopeshaji wake wa kimataifa.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo Ugiriki itapatiwa mkopo mwingine. Lakini Bunge la nchi hiyo linatarajiwa kupiga kura Alhamisi ijayo ili kuamua juu ya mapatano hayo ya kupatiwa Euro Bilioni 85 katika kipindi cha miaka mitatu.

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Annika Breidhardt amesema makubaliano katika kiwango cha kitaalamu yamefikiwa baina ya wajumbe wa wakopeshaji wa kimataifa na wa serikali ya Ugiriki baada ya mazungumzo ya wiki kadhaa.Lakini amesema bado yapo masuala fulani madogo madogo yanayoposwa kukamilishwa.

Juncker ashauriana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker leo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande na hapo jana alizungumza na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble. Ugiriki na wakopeshaji wake wa kimataifa ,wanatarajiwa kuyakamilisha makubaliano hadi ifikapo tarehe 20 ya mwezi huu wakati ambapo Ugiriki itapaswa kuilipa Benki Kuu ya Ulaya kiasi cha Euro Bilioni 3.4.

Belgien PK EZB Ecofin-Treffen der Finanzminister Wolfgang Schäuble
Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Pande tatu zinazofanya mazungumzo na Ugiriki ni Umoja wa Ulaya,Benki Kuu ya Ulaya,ECB na Shirika la fedha la Kimataifa IMF. Afisa mmoja wa wizara ya fedha nchini Ugiriki ameliambia shirika la habari la AFP kwamba masuala yaliyobakia hayatayaathiri makubaliano ya kimsingi yaliyofikiwa kwenye mazungumzo baina ya Ugiriki na wadai wake wa kimataifa.

Soko la hisa lapanda

Wakati Bunge la Ugiriki linatarajiwa kupiga kura juu ya mapatano ya kuiokoa nchi hiyo, soko la hisa la Athens lilipanda kwa asilimia 1.3

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amefahamisha kuwa mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro watakutana Ijumaa ijayo ili kuyaidhinisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya Ugiriki na wakopeshaji wake wa kimataifa. Waziri Mkuu Rajoy amesema Bunge la nchi yake litapiga kura kuunga mkono mpango huo wa tatu wa kuiokoa Ugiriki.

Nchini Ugiriki serikali ya nchi hiyo imefahamisha kwamba wakopeshaji wamekubali kufanya marekebisho ya kiasi fulani katika malengo ya bajeti yatakayaochangia katika kuleta ustawi wa uchumi na kuokoa kiasi cha Euro Bilioni 20. Serikali ya Ugiriki pia imearifu kwamba mabenki ya nchi hiyo yatapatiwa Euro Bilioni 10 za haraka.

Hata hivyo gazeti la "Kathimerini" limeripoti kwamba Ugiriki itapaswa kuchukua hatua 35 ili iweze kupatiwa msaada wa tatu.Ugiriki inatakiwa ifanye mageuzi katika sekta za nishati,mfumo wake wa kijamii na pia inatakiwa ifanye mageuzi yaliyopendekezwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afpe,ratre

Mhariri: Iddi Ssessanga