1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Geneva kuhusu Iran yatia matumaini

5 Desemba 2013

Mkataba wa Makubaliano ya Geneva kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia, uliofanyika siku kumi zilizopita, unaonekana kuwa wa mafanikio na kutoweza kuvurugwa na wabunge wa Congress Marekani, wanaounga mkono siasa za Israel.

https://p.dw.com/p/1ATpF
Wananchi wa Iran wakiwa na mabango ya kumpokea Rais Rouhani kutoka Geneva Nov 2013
Wananchi wa Iran wakiwa na mabango ya kumpokea Rais Rouhani kutoka Geneva Nov 2013Picha: picture-alliance/AP Photo

Licha ya kuwa kuna manung'uniko yasiyo ya msingi, kutoka katika chama cha Republican na Democratic kuhusu utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mkataba huo kati ya Tehran na mataifa makuu sita, wabunge hao wa Marekani hawana nguvu tena ya kupitisha maagizo mengine ya kuiwekea Iran vikwazo, kama ilivyokuwa inashinikizwa na Waziri mkuu wa Israel na wapambe wake.

Tehran imeweka wazi kuwa, vikwazo vyovyote vipya vitakavyopitishwa sasa, hata kama utekelezaji wake utaanza miezi sita baada ya mkataba wa sasa kuisha muda wake, utakuwa umekiuka masharti ya makubaliano ya sasa, na kuvuruga kabisa jitihada zote za kidiplomasia zilizokuwa zikifuatiliwa kwa miongo kadhaa, za kuhakikisha mpango wa Iran wa nyuklia hautawafanya kufikia kutengeneza silaha.

Msimamo wa Congress dhidi ya Iran kudhoofu

Msemaji wa ikulu ya Marekani- Jay Carney, alipozungumza na waandishi wa habari wiki hii alisema, endapo bunge lao litapitisha vikwazo vipya dhidi ya Iran ni wazi Iran na mataifa washirika wa Marekani, wataona kuwa Marekani waliingia katika makubaliano hayo kwa nia mbaya.

John Kerry na Sergei Lavrov, walipokutana Geneva katika mazungumzo kuhusu Iran
John Kerry na Sergei Lavrov, walipokutana Geneva katika mazungumzo kuhusu Iran Nov 2013Picha: Reuters

Kwa ujumla mfululizo wa kura za maoni zilizokusanywa kabla ya mazungumzo ya makubaliano dhidi ya Iran hayajaanza na baadaye, zinaonyesha kuwa wengi wameunga mkono hatua za kidiplomasia zilizochukuliwa kuliko zingefanyika nguvu za kijeshi.

Wamarekani wamechoshwa na vita kati yao na Mashariki ya kati

Katika duru la kwanza la ukusanyaji wa kura za maoni kwa watu mbalimbali huko Washington, baada ya mazungumzo ya hivi sasa kuhusu Iran, kupitia televisheni ya CNN, inaonyesha asilimia 64 ya watu wanakubaliana na muafaka wa kupunguza vikwazo vya kiuchumi kwa Iran, na kuona kuwa, itawawia vigumuTehran kutengeneza silaha, ambapo kwa upande wa maoni yaliyokusanywa na mashirika ya habari ya REUTERS na IPS yanaonyesha kuwa, wanaounga mkono maafikiano ya mkataba huo wa Iran kwa asilimia 44 dhidi ya asilimia 22.

Kwa ujumla wa matokeo yote, zaidi ya asilimia 68 ambayo ni sawa na theluthi mbili, wanakubaliana na mashauri ya kuwa, bunge la Marekani lisichukue hatua zozote zitakazozuia mafanikio ya makubaliano ya mkataba dhidi ya Iran, ambapo asilimia 21 tu ndo wanataka wabunge wa Marekani ikiwezekana wapitishe vikwazo vipya,bila kujali iwapo itavunja masharti ya mkataba mpya.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Zarif, akitoka katika mazungumzo ya Geneva
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Zarif, akitoka katika mazungumzo ya Geneva Nov 2013Picha: picture-alliance/dpa

Kutokana na matokeo ya maoni hayo,inaonyesha wazi kuwa wamarekani hawataki taifa lao kuingia tena katika vita nyingine na Mashariki ya kati.

Msimamo wa Israel na Makubaliano ya Geneva dhidi ya Iran

Licha ya kuwa waziri mkuu wa Israeli, Netanyau bado haridhii makubaliano hayo, lakini kimya kimya, wiki iliyopita amepeleka ujumbe wake maalumu Marekani ukiongozwa na mshauri wake wa masuala ya kiusalama, kukutana na uongozi wa rais Barack Obama, kwa ajili ya kujadiliana, nini kifanyike kwa makubaliano ya baadae ya dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Jumanne wiki hii, viongozi tisa wa ngazi ya juu waliokuwa katika serikali ya Israeli na mabalozi sita wa nchi mbalimbali waliopo Israel, walipeleka barua ya pamoja kwa wajumbe maalumu wa kamati ya taifa ya usalama katika bunge la Marekani, iliyoupongeza uamuzi wa mazungumzo ya Geneva.

Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Abdul-Rahman