1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamu wa rais wa Marekani asema hataitumia ibara ya 25

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
13 Januari 2021

Rais wa Marekani Donald Trump akiwa bado anazipinga lawama dhidi yake juu ya ghasia zilizofanywa na wafuasi wake kwenye majengo ya bunge la Marekani, nyufa zimejitokeza ndani ya chama chake cha Republican.

https://p.dw.com/p/3ns4j
USA US-Vizepräsident Mike Pence und Donald Trump
Picha: Carlos Barria/REUTERS

Makamu wa Rais Mike Pence amempa uzima rais Trump kwa kusema hataitumia ibara ya 25 inayomruhusu makamu huyo wa rais pamoja na baraza la mawaziri kumvua madaraka rais endapo ameshindwa kutimiza majukumu yake. Pence amesema haamini iwapo hatua hiyo itaafikiana na maslahi ya taifa.

Pence amesema hayo katika barua aliyomwandikia spika wa bunge Nancy Pelosi. Hata hivyo baraza la wawakilishi limetoa lawama kali kwa rais Trump kwa kupiga kura katika msingi wa chama kumtaka Pence achukue hatua ya kumwondoa rais madarakani.

Kutokana na Pence kukataa kuitumia ibara ya 25 ya katiba, sasa ni jambo la uhakika kwamba bunge linalodhibitiwa na Wademocrats litapiga kura ya kupitisha mashtaka juu ya kumng'oa Trump madarakani.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Donald J. Trump via Twitter/REUTERS

Wabunge hao watapiga kura leo. Mashtaka hayo ni juu ya hotuba ya Trump ya kuchochea maasi ya kutumia nguvu. Katika hotuba aliyotoa tarehe 6 mwezi huu Trump alidai kwamba yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi wa rais uliofanyika mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita.

Hotuba ya Trump

Katika hotuba hiyo Trump aliwachochea wafuasi wake kwenda kwenye jengo la bunge na kupambana. Mashtaka dhidi ya Trump yanatarajiwa kuungwa mkono na wajumbe wengi. Spika wa Bunge Nancy Pelosi amesema vitendo vya rais vimethibItisha dhahiri kushindwa kwake kutimiza majukumu na wajibu wake wa msingi, na kwa hivyo rais huyo lazima aondolewe mara moja kwenye madaraka yake. Hata hivyo; hailekei iwapo baraza la seneti linalodhibitiwa na wajumbe wa chama Trump cha Republican wataunga mkono kumweka rais huyo kikaangoni kabla ya kumaliza siku zake madarakani tarehe 20 Januari ambapo rais mteule Joe Biden anatarajiwa kuapishwa rasmi.

Katika upande mwingine maseneta kadhaa wa chama chake wameruka kambi na huenda wakaungana na wajumbe wa chama cha Democratic katika kupiga kura ya kuunga mkono mashtaka juu ya kumwondoa Trump madarakani. Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la New York Times kiongozi wa baraza la seneti linalodhibitiwa na Republican Mitch McConell amesema faragha kwamba Trump anastahili kushtakiwa kutokana na vitendo vyake.

Wakati huo huo, maafisa wa jeshi wa ngazi za juu wameshutumu matumizi ya nguvu ya wafuasi wa Trump wenye itikadi kali za mrengo wa kulia na wamethibitisha kwamba Joe Biden atapishwa wiki ijayo.