Makampuni zaidi ya 20 yakubali kupunguza utoaji hewa ukaa
2 Oktoba 2023Rais wa mkutano ujao wa Kimataifa kuhusu hali ya hewa,wa COP 28,Sultan al Jaber amesema makampuni zaidi ya 20 ya mafuta na gesi yameridhia mwito wake wa kuhimiza kupunguzwa kwa viwango vya hewa ukaa inayozalishwa na makampuni.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mkutano mkubwa wa kila mwaka wa sekta ya mafuta na gesi katika Umoja wa Falme za kiarabu,uliofanyika Jumapili.
Mkutano wa makampuni ya mafuta na gesi umetowa mwanga kwa kiasi fulani wa kile kinachoweza kutarajiwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa utakaofanyika mwezi Novemba huko Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mkutano huo wa makampuni ya mafuta na gesi ulikuwa na lengo la kuwakusanya wadau wakuu katika sekta hiyo kutangaza misimamo yao na kutowa ahadi ya kukubali kupunguza uzalishaji wa gesi ya Kaboni inayochafua mazingira,hatua ambayo itasaidia katika kupunguza ongezeko la joto duniani.
Kufuatia mkutano huo rais wa mkutano wa COP28 Sultan al Jaber amesema amefanikiwa kuyashawishi makampuni zaidi ya 20 kukubaliana na mwito wake wa kutaka viwango vya uzalishaji gesi hiyo ya Kaboni vipunguzwe.
Afisa mtendaji mkuu wa COP28 Adnan Amin akizungumzia kuhusu matarajio kuelekea mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 amesema ikiwa makampuni ya gesi na mafuta yatakubali kusaini mkataba wa kupunguza uzalishani wa kaboni, itakuwa ni hatua kubwa sana ya mafanikio ya mkutano huo.
"Utakuwa ni mkutano wa kwanza wa COP,ikiwa tutafanikiwa katika hili,ambao kimsingi utatowa nafasi ya kuwepo uwezekano wa kupima kiwango cha hewa ukaa tutakayoipunguza''
Afisa huyo mwandamizi wa COP kutoka Umoja wa Falme za kiarabu ameutaja mkutano uliowakusanya wadau katika sekta ya mafuta na gesi kuwa pia nafasi muhimu kwa serikali kuongeza juhudi kupunguza viwango vya joto duniani huku ripoti zikionesha kwamba hadi sasa nchi za ulimwengu haziko katika mwelekeo wa kutimiza ahadi zao za kupunguza ongezeko la joto duniani kutopindukia nyuzi joto 1.5 katika kiwango cha Celsius.
Kujumuishwa kwa wajumbe wa sekta hiyo ya mafuta na gesi kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kuanzia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2021 uliofanyika Scotland,ambako kwa ujumla makampuni ya nishati yalilalamika kutengwa kwenye mkutano huo.
Katika mkutano wa mwaka huu rais wa mkutano huo Sultan al Jaber ambaye pia ni mkuu wa kampuni kubwa ya mafuta ya nchi hiyo ADNOC ameitolea mwito sekta ya nishati kujiunga katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na ameyahimiza makampuni hayo kuwa katika nafasi muhimu ya kupatikana suluhisho katika mapambano hayo,japokuwa kwa upande mwingine, sekta hiyo inaongeza uzalishaji ili kujipatia faida kutokana na kuongezeka kwa bei ya nishati duniani.
Ikumbukwe kwamba hata yeye mwenyewe uteuzi wake wa kuongoza COP 28 ulizusha utata kwasababu nchi yake ni mwanachama wa jumuiya ya OPEC ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.Mkutano huo wa kimataifa umepangwa kufanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12.