1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majirani wa Libya wapinga uingiliaji kati wa kigeni

Yusra Buwayhid
24 Januari 2020

Wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoka nchi zilizo jirani na Libya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas wamekutana Algiers Alhamisi, kutafuta suluhisho la kisiasa la kumaliza mzozo wa Libya.

https://p.dw.com/p/3WkLJ
Algerien Algier | Außenminister-Treffen mit Nachbarländern Libyens
Picha: picture-alliance/dpa/M. Fischer

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas amewatolea wito majirani wa Libya kuunga mkono juhudi za kumaliza mgogoro uliodumu kwa karibu muongo mmoja katika taifa hilo la Afrika Kaskazini. Maas ameyasema hayo katika mkutano uliokutanisha viongozi wa ngazi za juu kwenye mji mkuu wa Algiers nchini Algeria. Maas amewaeleza wawakilishi wa Tunisia, Algeria, Niger, Sudan na Misri juu ya mazungumzo yaliyokutanisha makundi yanayozozana Libya na viongozi wa dunia na kujadili hatua za kupata suluhisho la kisiasa la kumaliza mgogoro huo.

Maas ameziambia nchi hizo jirani kwa Libya kwamba hamna anayeufahamu mzozo wa nchi hiyo ulioanza 2011 zaidi ya wao. Ameongeza kwamba vita hivyo vimekuwa vikichochewa na nchi za kigeni zenye nguvu ambazo zenyewe haziathiriki na vita hivyo.

"Ni majirani wanaoathirika zaidi na mzozo huu, kutokan na kuzuka makundi ya uhalifu, ugaidi, usafirishaji haramu wa silaha na binadamu, wakimbizi. Kwa hivyo ni muhimu zaidi kwa maslahi ya majirani wa Libya kupatikana amani na utulivu nchini Libya, " amesema Heiko Maas.

Libyen Tripoli 2019 | Kämpfer der GNA
Mwana´jeshi wa serikali halali ya (GNA) akipambana na vikosi vya Jenerali Khalifa HaftarPicha: picture-alliance/Xinhua News Agency

Majirani wa Libya wapinga uingiliaji kati wa kigeni

Washiriki wa mkutano huo walisisitiza juu ya haja ya kuiheshimu Libya kama nchi yenye umoja na kuheshimu uhuru wa mamlaka yake halali. 

"Ninapinga uwepo wa vikosi visivyo halali, haijalishi, ikiwa ni vya Libya au nchi zingine. Nchi ikiwa ina uhuru, basi inaweza kufanya makubaliano na yeyote yule. Lakini tunaogopa kwamba kuhusika kwa mataifa ya kigeni nchini Libya kutatatiza mambo zaidi, " amesema Sabri Boukadoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria akiwa na waandishi habari baada ya mkutano huo.

Mbali na kupinga uingiliaji kati wa nchi za kigeni, majirani hao wa Libya wamezisisitiza pande zote nchini humo kusuluhisha mgogoro wao kwa njia za amani.

Boukadoum amesema wanaamini kwamba watu wa Libya wanao uwezo wa kuweka mbali tofauti zao wakati wa mazungumzo na kufikia suluhisho la kisiasa. Ameongeza kwamba Umoja wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa washiriki pia katika kupatikana suluhu hiyo.

Katika mkutano wa mjini Berlin wa Jumapili, viongozi wa dunia walikubaliana kutekeleza marufuku ya Umoja wa Mataifa ya kujizuia kusambaza silaha. Lakini mahasimu wawili - Waziri Mkuu wa serikali halali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa Fayez al-Sarraj na Jenerali aliyegeuka kuwa mbabe wa kivita Khalifa Haftar - walikataa kuonana ana kwa ana mjini Berlin.

Vyanzo: (afp,ap)