1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Uturuki yadhibiti vijiji zaidi Syria

11 Oktoba 2019

Majeshi ya Uturuki yamefanikiwa kuvinyakua vijiji viwili zaidi vilivyokuwa vinashikiliwa na wanamgambo wa Kikurdi katika siku ya tatu ya operesheni ya kijeshi inayofanywa na nchi hiyo kaskazini mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3R9au
Syrien Tal Abyad Militäroffensive der Türkei
Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Shirika la habari la Uturuki, Anadolu limetangaza leo kuwa vikosi vya upinzani vinavyoungwa mkono na Uturuki pamoja na majeshi ya Uturuki vimevidhibiti vijiji vya Tal Hafer na Asfar Nejjar karibu na mji wa Ras al-Ayn. Vijiji 13 vilivyoko Tal Abyad na Ras al-Ayn vilidhibitiwa siku mbili zilizopita.

Uturuki imesema inakusudia kwenda umbali wa kilomita 30 kaskazini mwa Syria kuvisambaratisha vikosi vya Kikurdi na kuanzisha kile ilichokiita ''eneo salama.'' Anadolu imesema raia wawili zaidi wameuwa katika shambulizi la kombora kwenye mji wa Suruc na mwingine amekufa kutokana na majeraha ya shambulizi kama hilo lililotokea jana.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper ameitaka Uturuki kuacha kuendeleza operesheni yake ya kijeshi nchini Syria na kuionya kuwa inaweza kukabiliwa na madhara makubwa. Akizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar, Esper amesisitiza kuwa wanathamini uhusiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, lakini uvamizi huo unaweza kusababisha madhara.

Pakistan yaiunga mkono Uturuki

Katika hali isiyo ya kawaida, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan ametoa ahadi ya kuunga mkono uvamizi wa Uturuki nchini Syria. Taarifa iliyotolewa na serikali imeeleza kuwa Khan amempigia simu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kuelezea namna anavyomuunga mkono na kuonyesha mshikamano.

Khan amesema anaomba juhudi za Uturuki ziimarishe usalama, utulivu wa kikanda na suluhisho la amani kwa watu wa Syria liweze kufanikiwa kabisa. Erdogan anatarajiwa kuizuru Pakistan baadaye mwezi huu.

Türkei Grenzstadt Akcakale | Frauen flüchten vor Raketenangriff
Wanawake wakikimbia baada ya roketi kurushwa kwenye mji wa AkcakalePicha: Reuters

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk amesema operesheni ya Uturuki inaleta wasiwasi mkubwa na ameitaka nchi hiyo kuacha uchochezi wake wa kijeshi kabla hali hiyo haijasababisha janga lingine la kibaadamu.

''Wasiwasi wa kiusalama wa Uturuki unapaswa kushughulikiwa kwa njia za kidiplomasia na kisiasa. Uvamizi wa kijeshi utayafanya mambo kuwa magumu zaidi. Badala ya kuleta utulivu, itasababisha kukosekana kwa utulivu katika ukanda wote, raia wataumia zaidi, itasababisha watu kuyakimbia makaazi yao na kutishia hatua zilizopigwa na muungano wa kimataifa wa kijeshi katika vita dhidi ya Dola la Kiislamu,'' alisema Tusk.

Pendekezo la wakimbizi la Uturuki lakosolewa

Tusk amekosoa vikali pendekezo la Rais Erdogan kwamba atawapeleka wakimbizi milioni 3.6 wa Syria wanaoishi nchini Uturuki kwenye nchi za Ulaya hadi hapo Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 watakapoacha kusema hatua ya Uturuki kama ni uvamizi wa kijeshi.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 70,000 tayari wameyakimbia makaazi yao tangu Uturuki ilipoanzisha operesheni hiyo. Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP watu hao wamekimbia katika majimbo ya Al Hassakeh na Al-Raqqa.

Msemaji wa WFP amezikumbusha pande zinazohasimiana kwamba Umoja wa Mataifa unahitaji kuendelea kuwafikia watu 650,000 walioko kaskazini mashariki mwa Syria, ambao bado wanategemea msaada wa chakula.

Wakati huo huo, Uturuki imewakamata watu 121 kutokana na kuchapisha taarifa zinazoikosoa vikali Uturuki kuanzisha operesheni ya kijeshi Syria. Karibu watu 500 wanahojiwa kutokana na taarifa hizo.

(DPA, AP, AFP)