1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Syria yajibu mashambulizi

20 Machi 2017

Majeshi ya serikali ya Syria yamezima jaribio la waasi na makundi yenye itikadi kali za Kiislamu la kutaka kuiteka wilaya ya Jobar huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya mazungumzo mapya ya amani kuanza tena.

https://p.dw.com/p/2ZXEl
Syrien Kämpfe im Osten von Damaskus ausgebrochen
Picha: Getty Images/AFP/M. Eyad

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa baina ya serikali na waasi mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita lakini mapigano yamekuwa yanaendelea katika sehemu mbali mbali nchini Syria. Kwa mujibu wa waangalizi wa vita vya nchini Syria, mapigano makali yalizuka mapema leo ambapo vikosi vya serikali vilijibu mashambulio hayo kutokana na waasi kuendelea kusonga mbele na kuingia katika eneo la kaskazini mashariki mwa Damascus.

Shirika la kutetea haki la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema mapigano makali bado yanaendelea katika wilaya za Jobar na Al-Qaboun zilizo kasakzini mashariki mwa mji mkuu wa Damascus. Mkuu wa shirika hilo la kutetea haki nchini Syria Rami Abdel Rahman amesema vikosi vya serikali na washirika wake vinapambana na makundi yaliyoanzisha mapigano hayo hapo jana. Waasi nchini Syria wakishirikiana na makundi ya wapiganaji wa Jihadi waliokuwa hapo awali wanaongozwa na kundi la Fateh al-Sham lililokuwa na mahusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda walifanya mashambulizi katika maeneo yanayoshikiliwa na serkali katika wilaya ya mashariki ya Jobar kabla ya kuendelea na kuingia katika eneo la Abbasid. Hii ilikuwa ni mara kwanza kwa waasi kuingia katika eneo hilo la Abbasid katika kipindi cha miaka miwili lakini vikosi hivyo vya waasi vilikumbana na upinzani mkali wa vikosi vya serikali ambavyo vilifaulu kuwatimua waasi hao.

Wakati huo huo balozi wa Urusi nchini Syria Alexandar Kinshckak amesema jengo la ubalozi wa Urusi katika mji wa Damascus limeharibiwa kutokana na mapigano hayo baina ya vikosi vya serikali na waasi.

Schweiz Genf Staffan de Mistura
Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya Syria Staffan de Mistura anayesimamia mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria anatarajiwa kuanzisha tena mazungumzo hayo tarehe 23 mwezi huu baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Geneva tarehe 3 mwezi huu. Shirika la habari la Urusi RIA limesema naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Bogdanov ameelezea kuwa De Mistura atazuru Moscow kabla ya mazungumzo hayo kuanza na kwamba ana imani kuwa wawakilishi wa makundi ya waasi nchini Syria watahudhuria mazungumzo hayo yanayolenga kumaliza vita vya miaka sita. Majeshi ya Syria na washirika wake Urusi na Iran yameendelea kuwazidi nguvu waasi kwa kipindi cha miezi 18 sasa ijapokuwa waasi bado wanashikilia wilaya ya Ghouta iliyo mashariki mwa mji mkuu wa Damascus na baadhi ya wilaya za kusini na kaskazini mashariki mwa mji huo mkuu wa Damascus.

Mwandishi Zainab Aziz/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman