Majeshi ya Israel yavamia Gaza
4 Januari 2009Askari hao wa Israel wakiwa wamevalia miwani za kuona usiku huku wakiwa wamejipaka rangi usoni ,walivamia Gaza usiku, ambapo katika mapambano na wapiganaji wa Hamas watu tisa waliuawa wakiwemo wapiganaji watano wa Hamas, na kufanya idadi ya wapalestina waliyouawa mpaka sasa toka kuanza kwa mashambulizi hayo kufikia zaidi ya 450.
Hakuna taarifa zozote kuhusiana na madhara kwa upande wa Israel.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak alisemm kuwa hatua ya kuvamia Gaza ni katika kutimiza malengo ya kuyasambaratisha makundi yanayoshambulia kwa maroketi Israel.
Lakini msemaji tawi la kijeshi la Hamas, Abu Ubaida ameonya kuwa majeshi hayo ya Israel yatakabiliwa na kifo au kutekwa, na kwamba Israel kamwe haitoshinda vita hiyo.
Mjini New York Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao cha dharura kujadili hali katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert alitaka kusitishwa haraka kwa mashambulizi hayo ya ardhini ya Israel.
Nchi kadhaa duniani zimetoa wito kama huo wa Israel kusitisha operesheni yake hiyo ya uvamizi huko Gaza, huku maandamano yakifanyika katika miji mbalimbali barani Ulaya kulaani mashambulizi hayo ya Israel.
Umoja wa Ulaya, kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Czech ambayo ndiyo inayokalia kiti cha uongozi cha umoja huo,Karel Schwarzenberg, umeitaka Israel kutilia maanani maisha ya raia wakati wa operesheni zake hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Miguel Angele Moratinos mbali ya kutaka kusitishwa kwa operesheni hiyo, alitaka pia kusitishwa mara moja kwa mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel.
Hata hivyo kwa upande wake Rais George Bush wa Marekani katika hotuba yake kwa njia ya radio, hakuishutumu moja kwa moja Israel, na badala yake alilishutumu kundi la Hamas kwa kuwa chanzo cha hali hiyo.
Kwa upande mwengine juhudi za kidiplomasia kushughulikia hali hiyo zimekuwa zikiendelea, ambapo Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ambaye ni mjumbe maalum wa kundi la pande nne linalotafuta amani mashariki ya kati, anatarajiwa kuwasili hii leo kwenye eneo hilo.
Naye Rais Nicolaus Sarkozy wa Ufaransa anatarajiwa kuwasili kesho huko Misri kabla ya kwenda Ramallah na Jerusalem ikiwa ni katika juhudi hizo za kidiplomasia katika mzozo huo.
Duru za kidiplomasia zinasema kuwa mataifa ya Ulaya yanaanda rasimu ya mpango mpya wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.