1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Majenerali hasimu wa Sudan wakubali kukutana ana kwa ana

11 Desemba 2023

Majenerali hasimu wa Sudan Abdel-Fattah Burhan na Mohammed Hamdan Dagalo, wamekubali kukutana ana kwa ana kama sehemu ya juhudi za kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo ya kisiasa kumaliza vita vibaya nchini humo

https://p.dw.com/p/4a0TT
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan akitoa hotuba kwa taifa mnamo Agosti 14, 2023
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: Sudanese Army/AFP

Taarifa iliyotolewa jana na Jumuiya ya IGAD, imesema majenerali hao wawili wamekubali kusitishwa kwa mapigano bila masharti yoyote na kutatuliwa kwa  mgogoro ulioko kupitia mazungumzo ya kisiasa na pia kufanya mkutano wa ana kwa ana. Burhan, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza huru la utawala la Sudan, alihudhuria mkutano huo wa Jumamosi nchini Djibouti ambayo inashikilia urais wa kupokezana wa jumuiya hiyo ya IGAD. Wakati huo huo, Dagalo, ambaye hakuna hajulikani alipo, alizungumza kwa njia ya simu na viongozi wa IGAD.

Taarifa hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu lini na wapi majenerali hao wawili watakutana.

Soma pia: Mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan yakwama Jeddah

Alexis Mohamed, mshauri wa rais wa Djibouti, amesema jana kupitia mtandao wa X ambao awali ulijulikana kama twitter kwamba, majenerali hao wa Sudan walikubali mpango wa kukutana ndani ya siku 15 ili kutoa fursa ya mfululizo wa mikakati ya kujenga imani ambayo hatimaye itasababisha kufanywa kwa mazungumzo ya kisiasa ili kutamatisha mgogoro nchini humo.

Hakukuwa na jibu la haraka kutoka kwa jeshi la Sudan ama wanamgambo wa RSF.

Marekani yapongeza hatua ya Burhan na Dagalo kukubali kukutana

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Matthew Miller, amesema utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umepongeza kujitolea kwa majenerali hao wawili kusitisha mapigano na pia kukubali mkutano wa ana kwa ana huku ukiwatolea wito wawili hao kuzingatia kuanza mazungumzo bila kuchelewa.

Kiongozi wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Daglo wakati wa mazungumzo kati ya serikali ya mpito na kikosi hicho yaliosimamiwa na Sudan Kusini mjini Juba, mnamo Septemba 9, 2019
Kiongozi wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan DagloPicha: Akuot Chol/AFP

IGAD ni sehemu ya juhudi za upatanishi za kumaliza mzozo, pamoja na Saudi Arabia na Marekani ambazo zilisimamia duru kadhaa za mazungumzo yasio ya moja kwa moja kati ya pande zinazozozana nchini humo.

Umoja wa Mataifa wasema takriban watu milioni 25 wanahitaji msaada nchini Sudan

Umoja wa Mataifa umeweza tu kufikia sehemu ndogo ya karibu watu milioni 25 wanaohitaji msaada nchini Sudan inayokumbwa na mapigano. Haya ni kulingana na mratibu wa msaada wa kiutu wa Umoja huo kwa Sudan Clementine Nkweta-Salam.

Nkweta-Salam ameliambia shirika la habari la AFP kwamba msaada kwa hata watu milioni 4 wanaoweza kuwafikia unaweza kukoma hivi karibuni ikiwa ukosefu wa ufadhili utaendelea.

Soma pia:UN: Nusu ya raia wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu

Nkweta -Salami amesema hali nchini Sudan, miezi minane baada ya mzozo kuanza, ''imekuwa janga''na kwamba licha ya juhudi kabambe za mashirika ya misaada ya kibinadamu na washirika, bado wanakabiliwa na changamoto kubwa.

Mratibu huyo ameongeza kuwa takriban watu milioni 7 wametoroka makazi yao nchini humo hii ikiwa idadi kubwa zaidi duniani. Nkweta - Salam amesema kuwa wamelemewa katika uwezo wa kushughulikia mahitaji ya idadi hiyo kubwa ya watu.

Wafanyakazi wa misaada wametaja mgogoro huo kuwa "vita vilivyosahaulika".