1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano ya WTO yaendelea Geneva

P.Martin28 Julai 2008

Mawaziri wa biashara wa nchi wanachama 35 muhimu katika Shirika la Biashara Duniani WTO wanaendelea na majadiliano yao Geneva,Uswissi katika juhudi ya kukamlisha mkataba mpya utakaofungua zaidi masoko ya biashara.

https://p.dw.com/p/ElAQ
Kenya's Deputy Prime Minister and Minister of Trade Uhuru Kenyatta answers journalists' questions during a press conference during the fifth day of the World Trade Organisation ministerial summit on trade liberalisation talks, at the World Trade Organization (WTO) headquarters, in Geneva, Switzerland, Friday, July 25, 2008. (AP Photo/Keystone, Salvatore Di Nolfi)
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Biashara wa Kenya,Uhuru Kenyatta akijibu masuala ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa WTO mjini Geneva,Uswissi.Picha: AP

Baada ya kuwa na majadiliano ya juma zima kufufua majadiliano yaliyokwama yakijulikana kama Duru ya Doha,hatimae wajumbe Jumapili usiku walikubaliana kuzingatia mapendekezo mapya ili waweze kukamilisha mkataba mpya wa biashara.Hata hivyo mkataba huo utahitaji kuidhinishwa na wanachama wote 135 wa WTO.

Mapendekezo mapya yanazingatia hofu za nchi zinazoendelea kuhusu usalama wa chakula,uwezo wa kuendesha maisha na kuendeleza maeneo ya mashambani.Hata hivyo,mapendekezo hayo mapya yamepingwa na baadhi ya nchi na hata kukosolewa vikali na mashirika ya kijamii.Kiini cha mivutano ni ule ushuru wa forodha utakaotozwa kwa bidhaa za kilimo na za viwandani pamoja na ruzuku inayolipwa na serikali kwa wakulima katika nchi tajiri.

Kwa upande mwingine,maoni ya nchi masikini zinazoagizia vyakula,yamegawika kuhusu mapendekezo ya mkataba mpya wa biashara duniani.Mabishano yanahusika na yale mazao yatakayotiwa katika fungu maalum pamoja na ule "mfumo maalum wa ulinzi wa bidhaa."Kuambatana na mapendekezo hayo mapya,nchi zinazoendelea zitaweza kujiepusha kutozwa ushuru kamili wa forodha kwa bidhaa zitakazowekwa katika fungu maalum.

Nchi zinazoinukia kama vile India,China na Indonesia zinataka kuhakikisha kuwa mamilioni ya wakulima wanaojipatia riziki kwa kilimo kidogo,hawatoathirika,masoko ya biashara yatakapokuwa huru zaidi.Wakati huo huo,nchi zingine zinazoendelea na zinazouza nje vyakula,kama vile Thailand na Uruguay zinaamini kuwa msingi wa ukuaji na maendeleo,ni kuziuzia nchi masikini mazao zaidi.

Lakini baadhi ya nchi za Kiafrika zinasema tatizo si uhuru zaidi wa masoko bali tatizo kuu ni ruzuku zinazolipwa kwa wakulima katika nchi tajiri.Nchi za Kiafrika zinazozalisha pamba kama vile Benin,Burkina Faso,Chad na Mali zimetoa wito kwa nchi zilizoendelea kiviwanda hasa Marekani,kupunguza malipo ya ruzuku kwa wakulima wao.Wajumbe wa nchi hizo za Kiafrika wanalalamika kuwa malipo ya ruzuku hushusha bei za pamba duniani na huwaadhibu wakulima wa pamba katika nchi masikini.

Lakini mjumbe wa Marekani katika majadiliano ya WTO mjini Geneva amesema,sehemu muhimu ya mkataba wo wote ule ni China kukubali kupunguza ushuru wa forodha.China ni mnunuzi mkubwa kabisa wa pamba duniani.Kwa maoni ya Susan Schwab,hatua kama hiyo itasaidia kufungua masoko mapya kwa wakulima wa nchi za Afrika Magharibi na hata Marekani.

Mzozo mwingine uliogubika majadiliano ya WTO unahusika na zao la ndizi.Jumapili Umoja wa Ulaya na nchi za Latin Amerika zinazouza ndizi katika nchi za nje,zilikubaliana kupunguza ushuru wa forodha unaotozwa na umoja huo.Lakini Cameroon ikizungumza kwa niaba ya ACP yaani nchi za Bara la Afrika na eneo la Caribbean na Pacifik imesema,maafikiano hayo hayawezi kukubaliwa kama yalivyo.Kwani kupunguzwa zaidi kwa ushuru wa forodha kwa nchi za Latin Amerika huenda ukateketeza kilimo cha ndizi katika nchi za ACP.

Nchini Cameroon,sekta inayohusika na kilimo cha ndizi ni muajiri mkubwa wa pili baada ya serikali.Maafisa wa Cameroon wanasema,kiwanda hicho husaidia kuzuia machafuko yaliyoteketeza baadhi ya nchi za Afrika ya Maghiribi katika miaka ya hivi karibuni.

Duru hii mpya ya majadiliano ya WTO ilianza Julai 21 na majadiliano hayo huenda yakaendelea hadi katikati ya juma hili.