1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maisha yaanza kurudi upya barani Ulaya

4 Mei 2020

Mamilioni ya watu barani Ulaya wanaanza kurudi kwenye maisha ya kawaida, baada ya wiki kadhaa za kujifungia ndani kwa khofu ya maambukizo ya virusi vya korona lakini wanakaribishwa na dunia ambayo si kama walivyoiwacha.

https://p.dw.com/p/3bkXO
Corona-Lockerungen in Europa Italien
Picha: picture-alliance/dpa/Abaca

Anga la rangi ya buluu linawakaribisha wakaazi wa mji mkuu wa Italia, Rome, katika dunia ambayo kamwe haitakuwa tena ile waliyoiwacha wiki kadhaa nyuma wakati walipolazimika kujifungia ndani kwa khofu za maambukizo ya virusi vya korona. Kuna mengi yaliyobadilika na ambayo huenda yasirejee tena kwenye hali ya zamani.

Italia, taifa la pili baada ya Marekani kwa kuwa na vifo vingi vya wagonjwa wa COVID-19, limeanza rasmi shughuli za uzalishaji mali siku ya Jumatatu (4 Mei) kwa kufunguwa viwanda na maeneo ya ujenzi.

Mikahawa nayo imefunguliwa, lakini kwa huduma za kuchukuwa tu chakula, huku mabaa na maeneo mengine ya starehe yakiendelea kufungwa.

Watu wanashauriwa kuepuka kutumia usafiri wa umma, na wachache wanaoutumia, wanalazimika kuvaa barakoa.

Uchumi wa Italia, ambao ni wa tatu kwa ukubwa katika Ukanda wa Euro, unatazamiwa kusinyaa katika kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu Mfadhaiko wa Kiuchumi wa Kilimwengu wa miaka ya 1930. 

Marekani yazidi kuishutumu China

USA | Washington | Trump äußert sich über das Coronavirus
Rais Donald Trump wa Marekani anaamini kuwa China inahusika na kusambaa kwa virusi vya korona duniani.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Kwa Marekani, taifa linaloongoza kwa maambukizo na vifo, inuko la kiuchumi lilikuwa liwe alama kuu ya mafanikio ya Donald Trump kwenye kampeni yake ya kuomba kuchaguliwa tena kuwa rais kwenye uchaguzi wa Novemba.

Lakini wiki kadhaa za zuio la shughuli za maisha limepelekea Wamarekani milioni 30 kupoteza ajira zao, na sasa kiwango cha uungwaji mkono kwa Trump kimeshuka. 

Mwenyewe Trump ameongeza mashambulizi yake dhidi ya China, akiituhumu kuwa chanzo cha kirusi ambacho anasema kilianzia kwenye maabara moja mjini Wuhan.

Kauli hiyo sasa inaungwa mkono na waziri wake wa masuala ya kigeni, Mike Pompeo, ambaye amesema ana ushahidi wa kutosha kuwa virusi vya korona ni zao la maabara za Kichina.

"Nadhani dunia nzima inaweza kuona sasa, na kumbuka, China ina historia ya kuuambukiza ulimwengu na kuendesha maabara zilizo chini ya viwango," alisema Pompeo siku ya Jumapili bila kutaja hasa kilipo chanzo cha ushahidi wake.

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani alisema kuwa bado wachambuzi wanachambua taarifa walizokusanya kujuwa asili hasa ya virusi hivyo.

Wanasayansi bado hawaamini China kuhusika

BdTD | Bild des Tages Deutsch | Graffiti in Berlin
Mchoro unaowaonesha marais wa China na Marekani wakibusiana katika wakati wa janga la COVID-19.Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

China, kwa upande wake, inakanusha madai hayo.

Hadi sasa wanasayansi wengi wanakubaliana kuwa ugonjwa wa COVID-19 ulitokana na jamii ya wanyama kwenda kwa wanaadamu kwa utaratibu wa kawaida wa kimaumbile.

Kurejea kwa kauli hizi dhidi ya China kutoka serikali ya Marekani kumeyatikisa masoko ya hisa hivi leo, huku wawekezaji wakiwa na wasiwasi endapo zinaweza kuishia kwenye vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo makubwa duniani.

Soko kuu la hisa la Hong Kong limeshuka kwa asilimia nne, huku mengine barani Asia yakipoteza asimilia mbili na ya Ulaya yakianza Jumatatu hii kwenye mstari mwekundu.

Kiasi cha watu 248,000 wamepoteza maisha yao tangu virusi vya korona kuibuka nchini China mwishoni mwa mwaka uliopita, na haraka sana kikaweza kusambaa kwenye mataifa mengine na kuwaambukiza watu wapatao milioni tatu na nusu.

Reuters, AFP