1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maisha marefu ya Robert Mugabe Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Februari 2017

Maisha marefu ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kushindwa mpango wa rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini wa kujitoa katika ICC na kitisho cha njaa barani Afrika ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2YBzU
Simbabwe Harare Präsident Robert Mugabe und Ehefrau Grace
Picha: Reuters/P. Bulawayo

"Maisha ya kila aina ya muimla Robert Mugabe" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la berliner Zeitung kuhusu maisha ya kiongozi huyo mkongwe kabisa anaendelea kung'ang'ania madaraka barani Afrika. Gazeti linajiuliza kama mkewe Mugabe, Grace, anamtakia mema. Bibi huyo mwenye umri wa miaka 51 alisema kiongozi huyo mkongwe  aliyesherehekea miaka 93 wiki hii , "anapendwa hadi na wananchi  kwa namna ambayo hata Mungu akimchukua, chama chake kitamchagua kugombea kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa miaka miwili kutoka sasa, na ana nafasi nzuri ya kushinda," anasema. Gazeti la Berliner Zeitung linazungumzia mkutano mkuu wa chama tawala ZANU/PF ulioitishwa decemba mwaka jana ambapo Robert Mugabe anaeitawala Zimbabwe tangu uhuru miaka 37 iliyopita , amechaguliwa kugombea tena wadhifa huo.

Akimudu kuingia mhula wa nane basi atakuwa na umri wa miaka 99 na kwa namna hiyo atavunja rikodi zote za dunia. Hata hivyo matamshi ya Grace Mugabe yanafichua kitu kimoja nacho ni kwamba hata yeye mwenyewe haamini miujiza. Kwasababu "Mjomba Bob" siku hizi anadhoofika zaidi kuliko hata jinsi uchumi wa nchi hiyo unavyodhoofika. Mzee huyo ameshawahi kuanguka na ameshawahi kusoma tangu mwanzo mpaka mwisho hotuba ambayo alikwisha isoma wiki chache kabla , linasimulia gazeti hilo baadhi tu ya ishara za kuzeeka Robert Mugabe. Pindi angeng'atuka baada ya miaka 20 madarakani, basi maisha yake ya uzeeni yangepata sifa ya kiongozi wa kuheshimiwa. Lakini kwa kung'ang'ania madaraka, ameiharibia hadhi mpaka nchi yake. Uchumi wa Zimbabwe umedhoofika kama alivyodhoofika kiongozi huyo aliyezeeka. Linamaliza kuandika gazeti la Berliner Zeitung.

Uamuzi wa serikali ya Afrika kusini kujitoa katika korti ya ICC ni batil

"Mpango wa Zuma umeshindwa" linaandika gazeti la Süddeutsche linalozungumzia uamuzi wa korti kuu ya mjini Pretoria unaoitaka Afrika Kusini isijitoe katika korti ya akimataifa ya uhalifu-ICC mjini The Hague. Korti hiyo inasema uamuzi uliopitishwa na serikali ya Afrika Kusini october mwaka jana  wa kujitoa katika korti ya ICC mwaka mmoja kutoka sasa ni "kinyume na katiba na batil". Rais Jacob Zuma anabidi haraka aibatilishe. Afrika Kusini inaweza kujitoa  tu ikipata idhini ya bunge. Serikali inadhamiria kuchunguza hatua ya korti kuu na kuona kama inaweza kukata rufaa. Zaidi ya hayo  chama tawala cha ANC kinadhibiti wingi wa viti bungeni kwa namna ambayo inaweza kusitisha ushirikiano na korti hiyo ya kimataifa.

Süddeutsche Zeitung limekumbusha kwamba Afrika Kusini chini ya uongozi wa marehemu rais Nelson Mandela ni miongoni mwa waasisi  wa korti hi kimataifa iliyoundwa mwaka 1998. Uhusiano kati ya korti hiyo  na mataifa kadhaa ya Afrika umeharibika miaka ya hivi karibuni huku baadhi ya serikali za Afrika zikiwalaumu majaji wa mjini The Hague kuwalenga zaidi viongozi wa Afrika. Umoja wa Afrika umeunga mkono mwishoni mwa mwezi uliopita, mataifa ya Afrika "kujitoa kwa pamoja" toka korti hiyo, lakini uamuzi huo si lazma kufuatwa, linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche .

Ukame waathiri bara la Afrika

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu janga la ukame barani Afrika. Lilikuwa gazeti hilo hilo la mjini Munich, Südeutsche lililomulika janga la ukame na kitisho cha njaa barani Afrika. Pekee Sudan Kusini watu zaidi ya milioni tano wanakumbwa na balaa hilo ambalo Süddeutsche linahisi chanzo chake kimesababishwa na binaadam. Balaa kubwa zaidi litapiga, linaandika gazeti hilo linaloitaja ripoti ya Umoja wa Mataifa inayozungumzia kitisho cha janga la ukame katika kanda ya Afrika kati na Afrika mashariki.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri:Yusuf Saumu