1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahujaji milioni mbili waanza safari ya Arafa

26 Juni 2023

Mahujaji wapatao milioni mbili wameanza rasmi hivi leo ibada ya kila mwaka ya Hijja baada ya kufanya tawafu ya kuizunguka nyumba tukufu kwa Waislamu iitwayo Kaaba katika mji wa Makkah nchini Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/4T48q
Saudi-Arabien, Mekka | BG Haddsch
Picha: Ashraf Amra/APAimages/IMAGO/APAimages

Mahujaji wa Kiirani waliwasili katika Msikiti Mtukufu wa Makkah wakiwa kwenye basi jipya, ishara ya jinsi maridhiano kati ya Iran na Saudi Arabia yalivyoimarisha huduma hizo za kila mwaka kwa waumini wanaotembelea eneo hilo takatifu kabisa kwa Waislamu duniani.

Sayyid Mahdi, anayesimamia mahujaji wapatao 2,800 wa Iran alisema mamlaka za Saudi Arabia zimewafanyia "ukarimu mkubwa kwa kuwatengea hoteli maalum" kwa ajili yao mwaka huu. 

Soma zaidi: Umati wa mahujaji umewasili mjini Makkah

Kwa ujumla, miongoni mwa mahujaji milioni mbili wanaofanya ibada hiyo mwaka huu, 87, 550 wanatokea nchini Iran, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kutoka nchi hiyo kwa miaka ya hivi karibuni.

Iran na Saudi Arabia, ambazo zimekuwa kwenye mzozo wa kisiasa na kidiplomasia kwa miongo kadhaa, zilifikia makubaliano ya kurejesha mahusiano yao mnamo mwezi Machi mwaka huu kufuatia juhudi za upatanishi zilizosimamiwa na China.

Mahujaji kutoka Sanaa wapokelewa

Mji wa Jeddah pia umewapokea mahujaji 270 waliowasili kwa ndege kutokea mji mkuu wa Yemen, Sanaa, ikiwa safari ya kwanza ya aina hiyo kwa zaidi ya miaka saba sasa, tangu Wahouthi kutwaa udhibiti wa mji huo.

Saudi-Arabien, Mekka | BG Haddsch
Mahujaji kutoka Sudan wakiwa kwenye Msikiti Mtukufu wa Makka.Picha: Sajjad Hussain/AFP/Getty Images

Mkuu wa Uwanja wa Sanaa, Khalid Al-Shayyef, alisema kuwa ndege hiyo ni moja kati ya tano ambazo zimewabeba mahujaji wa Yemen mwaka huu, ambapo nyengine zinatazamiwa kuwasili leo. 

Soma zaidi: Waislamu milioni 1 waanza Ibada ya Hajj

Saudi Arabia iliunda muungano wa kijeshi na kuivamia Yemen mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali iliyopinduliwa na wapiganaji wa Kihouthi mwaka 2014 na tangu hapo kumekuwa na vita vikali baina yao. 

Lakini kwa kipindi sasa, pande hizo mbili zimekuwa na majadiliano na ubadilishanaji mahabusu wa kivita unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa na safari ya mara hii ya mahujaji kutokea Sanaa ni miongoni mwa matokeo ya mchakato huo wa majadiliano.

Hijja ya kwanza baada ya janga la UVIKO-19

Hijja, ambayo ni moja kati ya matukio yanayokusanya watu wengi zaidi kwa wakati mmoja duniani, imerejea kwenye hali yake ya kawaida kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa janga la UVIKO-19 miaka mitatu iliyopita.

Ibada hiyo ni mojawapo kati ya nguzo tano za Uislamu na kila muumini wa dini hiyo mwenye uwezo anatakiwa kufanya safari ya siku tano ya Hajj angalau mara moja maishani mwake. 

Leo mahujaji wanaanza  safari yao kuelekea Uwanja wa Arafa katika safari wanayoamini ina uzoefu mkubwa wa kiroho, ambayo hufuta madhambi yao, kuwakurubisha kwa Mungu wao na kuwaunganisha na waumini wenzao zaidi ya bilioni 1.8 ulimwenguni. 

Vyanzo: AP, AFP, Reuters