Mahathir Mohamad ataka kuiongoza tena Malaysia
8 Januari 2018Mahathir Mohamad atakuwa ni kiongozi mwenye umri mkubwa kabisa duniani ikiwa muungano wa upinzani unaomuunga mkono utashinda katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti ingawa wachambuzi wanaamini kwamba hili sio rahisi kutokea. Kiongozi huyo muimla anayefahamika kwa ulimi wake mkali aliitawala Malysia kwa miaka 22 hadi mwaka 2003 na kumpfanya kuwa waziri mkuu aliyewahi kuiongoza nchi hiyo kwa muda mrefu zaidi.
Katika utawala wake aliwafunga wanachama wa upinzani bila ya kuzingatia sheria au kufunguliwa mashtaka kwa kisingizio cha kulinda usalama katika mwaka 1987 na kuonekana kuwa mtawala wa kiimla ambaye alizikanyaga haki za binadamu bila kujali. Na hata alipostaafu hakuchelelea kutoa amri kwa waliomrithi.
Na baada ya kuzuka madai kwamba kiwango kikubwa cha fedha kimeibiwa kutoka hifadhi ya fedha ya taifa iliyoundwa na waziri mkuu wa sasa Najib Razak alijiondoa katika chama tawala na kuvaa gwanda jipya la kisiasa ili kujaribu kumpindua mtu ambaye aliwahi kuwa mshirika wake aliyemuunga mkono na kumuongoza.
Wizara ya sheria ya Marekani inadai kwamba dolla bilioni 4.5 ziliibwa kutoka mpango wa uwekezaji katika kampeni ya wizi mkubwa na utakatishaji fedha nchini Malysia. Najib anakanusha kuhusika kwa hali yoyote katika tuhuma hizo huku pia akionekana kupambana kwa hali zote pamoja na kuwazima wakosoaji kutoka serikali yake na kuzuia uchunguzi wa ndani.
Maadui wa zamani sasa marafiki
Kurudi katika ulingo wa siasa kwa Mahathir kunatizamwa kwa jicho la mshangao na wale waliokuwa maadui zake na hata kiongozi wa upinzani anayeshikiliwa jela Anwar Ibrahim ikiwa ni kama mabadiliko ya aina yake ya mkondo wa siasa hasa kutokana na wanasiasa hao wawili Anwar na Mahathir kuwahi kuwa maadui wakubwa katika miongo mwili ya siasa zilizohodhiwa na watu hao wakati huo.
Anwar alikuwa mtu aliyetakiwa kisheria kurithi uongozi baada ya Mahathir hadi pale waziri mkuu huyo alipoamua kumfuta kazi mwaka 1998 baada ya kutofautiana kisiasa na kufungwa jela kwa kipindi cha miaka sita kwa tuhuma za kulawiti na kuhusika na vitendo vya rushwa.
Baada ya Anwar kuachiwa huru aliongoza upinzani na kuufikisha katika nafasi nzuri ambayo haijapata kuonekana katika uchaguzi wa mwaka 2013 lakini kwa mara nyingine akakamatwa na kutiwa jela mwaka 2015 chini ya utawala wa Najib.
Mahathir kumpisha Anuar Ibrahim
Anwar amekuwa akilaani hatua ya kushikiliwa kwake akisema imechochewa kisiasa. Baada ya Mahathir kukata ushirika na chama tawala cha United Malys National Organisation UMNO aliamua kurudisha usuhuba katika upande wa Anwar uliokuwa umevunjika ambapo viongozi hao walikutana mwaka 2016 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 18. Chama chake cha Bersatu kimejiunga na muungano wa upinzani ambao pia unakijumuisha chama cha Anwar na vingine vingi vinavyoongozwa na waliowahi kuwa wakati mmoja maadui zake.
Na jumapili iliyopita muungano huo kwa kauli moja umempitisha mtawala huyo wa zamani Mahathir Mohamad kugombea nafasi hiyo ya waziri mkuu. Hata hivyo endapo muungano huo wa UMNO utafanikiwa kushinda uchaguzi wa Agosti na kukiondoa chama kilichokaa madarakani tangu 1957 basi Mahathir atakuwa waziri mkuu wa muda na baadae Anwar kutwaa uongozi pale atakapoachiwa huru..
Mwandishi: Saumu Mwasimba/afpe
Mhariri: Mohammed AbdulRahaman