Mahasimu wa Syria wakutana ana kwa ana
25 Januari 2014Baada ya kuanza vibaya hapo Ijumaa pande hizo mbili zimekutana pamoja katika chumba hicho hicho na mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi katika makao makuu ya Umoja huo kwa bara la Ulaya.
Mkutano huo ambapo Brahimi tu ndiye aliyezungumza na ujumbe wa pande hizo mbili ukisikiliza ulimalizika katika kipindi kisichozidi dakika thelathini.Pande hizo mbili baadae zilihamia katika vyumba tafauti ambapo Brahimi alikuwa akitarajiwa kuwasaliana nao kwa zamu. Anas al Abda mjumbe wa upinzani amekaririwa akisema sio rahisi kwao kukaa na ujumbe wenye kuwakilisha wauaji mjini Damascus lakini wamefanya hivyo kwa matlaba ya watu wa Syria.
Kiongozi wa ujumbe wa serikali ambaye ni balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jaafari ameliambia shirika la habari la AFP kwamba yumkini ikabidi wazimeze chuki zao lakini wapo hapo na wako makini na wana maelekezo yalio wazi na mawazo yao yako wazi na yana nia njema.
Kukutana tena jioni
Umoja wa Mataifa umesema watarudi tena kwenye chumba hicho jioni hii kwa kikao ambacho wapinzani wanasema kitalenga masuala ya misaada ya kibinaadamu hususan hali katika mji uliozingirwa wa Holms lakini serikali imesema kikao hicho kitakuwa cha jumla.
Licha ya kikao chao kuwa cha muda mfupi mno, mkutano huo bado unaonekana kupiga hatua baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo magumu kushuhudia utawala wa Rais Bashar al -Assad ukiushutumu upinzani kwa kukwamisha mazungumzo hayo na kutishia kujiondowa.
Pande hizo zinakutanishwa pamoja kwa mara ya kwanza chini ya shinikizo zito la kidiplomasia la Umoja wa Mataifa, Marekani na Urusi kuwahi kushuhudiwa katika juhudi za kukomesha umwagaji damu wa Syria kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya takriban miaka mitatu.
Brahimi alitagaza hapo Ijumaa usiku kwamba pande hizo mbili zimekubali kukutana pamoja na kukiri kwamba mchakato huo ni mgumu.
Brahimi amewaambia waandishi wa habari kwamba katu hawakutegemea mchakato huu kuwa rahisi lakini amesema "nafikiri pande hizo mbili zinafahamu kile kilicho hatarini".
Tofauti bado ni kubwa
Upinzani umesisitiza kwamba mazungumzo hayo yanapaswa kulenga katika suala la kuondoka madarakani kwa Assad na kuundwa kwa serikali ya mpito kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa kwanza wa amani mjini Geneva hapo mwaka 2012.
Serikali inasema dhima ya Assad sio suala la mjadala katika mkutano huu uliopewa jina la Geneva Mbili na imekanusha kwamba makubaliano ya awali ya Geneva yanataka kiongozi huyo aondoke madarakani.
Matarajio ya kufikiwa kwa ufumbuzi katika mazungumzo hayo yanayotazamiwa kudumu kwa takriban wiki moja ni madogo lakini wanadiplomasia wamesema kule tu kuzikutanisha pande hizo mbili pamoja kwa mara ya kwanza ni hatua muhimu.
Anas al-Abda anataraji siku za kwanza au hata pengine wiki za mazungumzo pande hizo mbili zitazungumza tu kwa kupitia Brahimi.
Wakati ikionekana kwamba hakuna upande ulio tayari kuridhia masuala muhimu wasuluhishi wataelekeza juhudi zao katika kufikia makubaliano ya muda mfupi ili kuendeleza mchakato huo ikiwa ni pamoja na usitishaji wa mapigano wa maeneo, kufunguwa njia za kufikisha misaada ya kibinaadamu na kubadilishana wafungwa.
Imechukuwa juhudi za miezi kadhaa kuzishawishi pande hizo mbili kuhuhudhuria mkutano huo wakati Baraza la Kitaifa la upinzani likiamua dakika za mwisho kuususia mkutano huo.
Kuna mashaka iwapo ujumbe wa upinzani ni wawakilishi wa kweli wa wapinzani wa Assad na iwapo utaweza kutekeleza makubaliano yoyote yale na wapiganaji waasi walioko kwenye medani za mapambano ndani ya Syria kwenyewe.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri: Daniel Gakuba